May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sherehe Dar zapigwa ‘stop’ siku 21

Spread the love

 

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Aboubakar Kunenge amepiga marufuku kufanyika kwa sherehe yoyote ile ndani ya mkoa huo kwa kipindi cha siku 21 cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli (61). Anaripoti Kelvin Mwaipungu…(endelea).

Kunenge ametoa agizo hilo leo Ijumaa tarehe 19 Machi 2021, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini wake, ikiwa ni muda mchache kupita, tangu Mama Samia Suluhu Hassan, aapishwe kuwa Rais wa Tanzania.

Mara baada ya kumaliza kuapishwa, Mama Samia amesema, maombolezo ya kifo cha Hayati Magufuli, yatakuwa kwa siku 21. Ni kuanzia 17 Machi alipofariki hadi 9 Aprili 2021.

Mwili wa Dk. Magufuli utazikwa Alhamisi 25 Machi 2021, nyumbani kwake Chato mkoani Geita.

Akizungumza na waandishi wa habari, RC Kunenge amesema “nitoe rai, nitoe agizo, katika siku 21 hizo, hakuna sherehe yoyote itakayoruhusiwa kufanyika. Sisi ni waungwana, tuheshimu mila na desturi zetu za Watanzania. Huu ni msiba mkubwa, hatuwezi kuwa na sherehe zikiendelea.”

Katika kusisitiza hilo, RC Kunenge amesema “nitoe wito tena, hakuna sherehe yoyote itakayoruhusiwa katika kipindi cha siku 21.”

Kunenge ametoa ratiba na utaratibu wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Hayati Magufuli kwa wananchi wa mkoa huo uliopangiwa siku mbili za kutoa heshima za mwisho kati ya kesho na keshokutwa.

Amesema kesho Jumamos, kuanzia saa 1:00 -3:00 asubuhi itafanyika Misa takatifu kanisa Katoliki St. Petro, Saa 3:00 – 3:30 asubuhi, mwili utawasili Uwanja wa Uhuru, Saa 3:30 – 4:30 asubuhi itafanyika Misa takatifu ambapo Saa 4:30 asubuhi hadi saa 9: 30 alasiri viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, wafanyakazi na taasisi za umma watatoa heshima za mwisho na majira ya saa 9:30 – 12:00 wananchi watatoa heshima za mwisho.

Kunenge amesema, Jumapili saa 2:00 asubuhi mwili utawasili Uwanja wa Uhuru, Saa 2:30 asubuhi hadi saa 10:30 jioni, wananchi watatoa heshima za mwisho ambapo saa 10:30 jioni hadi saa 11:00 jioni mwili utaelekea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere ambapo saa 11:00 jioni adi Saa 11:45 jioni utasaririshwa kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma.

error: Content is protected !!