March 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Ponda: Nakwenda Hijja kusoma dua nzito

Spread the love

SHEIKH Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu anasema, anakwenda Hijja leo Agosti 02, 2018 pamoja na kutekeleza Nguzo ya Tano ya Kiislam pia atasoma dua nzito kwa ajili ya taifa. Anaandika Faki Sosi, … (endelea).

Kupitia taarifa yake aliyoituma kwenye vyombo vya habari leo Sheikh Ponda amesema kuwa, kwanza anakwenda kufanya ibada kama ilivyo kwa mahujaji wote Tanzania na duniani.

“Ninakwenda Hijja kutekeleza ibada ya Hijja kama nguzo ya Tano ya Kiislam. Kwangu na kwa Mwislam yoyote anapaswa kutekeleza hilo anapokuwa na uwezo.

“Kutokana na mwenendo wa taifa leo, kwangu nimeona ni firsa nzuri kuliombea taifa kwani mambo hayaende kama wengi tulivyotarajia. Kuna matukio mengi ya kuogopesha yanatokea na huenda yakaonekana kuwa ya kawaida hapo baadaye,” amesema Sheikh Ponda.

Sheikh Ponda amefafanua kuwa, nchi kwa sasa ipo kwenye wakati mgumu katika masuala ya haki, uchumi na kwamba, sasa ni fursa kumshtakia Allah kwa wale wanaotenda vitendo visivyo vya kibinaadamu.

“Natoa wito kwa mahujaji wengine wa Tanzania kuungana nami kwenye maombi ili Allah afanye wepesi kuinusuru nchi yetu.

“Hili lisiwe la Waislam pekee, kila mmoja na kwa Imani yake ni wakati sasa kumwelekea Mwenyezi Mungu kuhakikisha jambo hili analiondoa kwa namna anavyotaka yeye,” amesema Sheikh Ponda.

Miongoni mwa matukio anayotaja kuogofya ni pamoja na utekaji wa watu kiholela, mauaji ya raia wasio na hatia, vitisho kutoka kwa viongozi pamoja na kuminywa kwa uhuru wa habari na kujieleza.

“Kinachotutokea ama kinachofanywa na watawala kinatuathiri wote hivyo kila mmoja anawajibika kupinga kwa namna inayofaa,” amesema.

error: Content is protected !!