Thursday , 29 February 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Sheikh Ponda bado ang’ang’aniwa
Habari za SiasaTangulizi

Sheikh Ponda bado ang’ang’aniwa

Sheikh Ponda Issa Ponda
Spread the love

MWANAWAZUONI, mwanaharakati na kiongozi mashuhuri wa madhehebu ya dini ya Kiislamu nchini, Sheikh Ponda Issa Ponda, bado anaendelea kushikiriwa na jeshi la polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, anaripoti Faki Sosi.

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo na vyanzo vingine vya taarifa, akiwamo Sheikh Rajabu Katimba zinasema, Sheikh Ponda aliyeripoti polisi kwa hiari yake leo asubuhi, bado anaendelea kushikiriwa akituhumiwa “kufanya uchochezi.”

Sheikh Ponda aliwasili kituo kikuu cha Polisi Kati (Centro), majira ya saa nne asubuhi leo Ijumaa, akiwa ameongozana na jopo la mawakili wake watatu, akiwamo Prof. Abdallah Safari.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, miongoni mwa mashitaka anayotuhumiwa Sheikh Ponda, ni madai kuwa ametaka wananchi kutoviogopa vyombo vya dola, kuituhumu serikali kuhusika na vitendo vya mauaji ya raia na kutesa na kuteka watu mbalimbali.

Viongozi wandamizi wa jeshi la polisi nchini, walianza kumtafuta Sheikh Ponda tokea juzi Jumatano, kabla ya kuanza mkutano wake na waandishi wa habari, uliofanyika kwenye hoteli ya Iris, Kariakoo, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, Sheikh Ponda alieleza alichoita, “kutoridhika kwake na hatua ambazo jeshi la polisi inazichukua katika kufanya upelelezi wa matukio mbalimbali, ikiwamo kushambuliwa kwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.

Aidha, Sheikh Ponda alidai kuwa ameamua kuitisha mkutano huo, kutokana na kile alichoita, “kupokea wosia” wa Lissu, wakati alipokwenda kujulia hali mjini Nairobi anakopatiwa matibabu ya majeraha ya risasi.

Lissu amelazwa katika hospitali kuu ya Nairobi kwa takribani mwezi mmoja na siku saba sasa, akipatiwa matibabu na madaktari bingwa zaidi ya 10 wanaozunguuka kitanda chake kila siku, kufuatia kushambuliwa kwa risasi za moto na wanaoitwa na serikali, “watu wasiofahamika.”

Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mnadhimu wa Kambi rasmi ya upinzani bungeni, mwanasheria mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 40, majira ya saa saba na nusu mchana, tarehe 7 Septemba mwaka huu, nje ya nyumba yake, Area D, mjini Dodoma.

Lissu alikuwa akirejea nyumbani kutokea bungeni, ambako alishiriki mjadala wa mkutano wa asubuhi. Lissu alinusurika kifo, wiki mbili baada ya kunukuliwa akisema, “maisha yangu yako hatarini.”

Kwa mujibu wa Sheikh Ponda, hali ya Lissu kwa sasa inaendelea vizuri. Anasema, yeye binafsi alipata fursa ya kuzungumza naye kwa kina na kujadiliana naye juu ya mustakabali wa nchi.

Anasema, ni katika mazungumzo ambayo yamemsababishia kushikiriwa na jeshi la polisi baada ya kuamua kuyaweka hadharani, Lissu amemueleza, “damu yangu na yako zilizomwagika, hazitakwenda bure.”

Sheikh Ponda ambaye pia ni katibu mkuuwa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, alinusurika kukamatwa na polisi baada kuondoka kwenye eneo ambalo alikuwa anakutana na waandishi wa habari, mithili ya mtu “aliyetonywa.”

Polisi walifika eneo hilo muda mfupi baada ya Sheikh Ponda kuondoka. Baada ya kumkosa Sheikh Ponda, waliamua kuwakamata waandishi waliohudhuria mkutano wake.

Kufuatia kushindwa kumtia mbaroni Sheikh Ponda kwenye eneo hilo, jana (Alhamisi) Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, alimtaka Sheikh Ponda kujisalimisha mwenyewe polisi.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari, alioufanya siku moja baada ya kurejea nchini kutokea Nairobi, Sheikh Ponda alisema, “nimeguswa na maneno ya Lissu. Ameniambia, tusiogope na kwamba damu yetu iliyomwagika, haitakwenda bure.”

Sheikh Ponda amesema, “tulipokuwa tunabadilisha mawazo, niliguswa mno. Nimepata hisia kubwa. Badala ya mimi kumpa matumaini, yeye ndiye aligeuka na kunipa matumaini.”

Amesema alikwenda Nairobi kumjulia hali Lissu, kumwombea dua, kumjengea matumaini ya afya na kupata taarifa za kina ya kilichotokea kutoka kinywani mwa Lissu mwenyewe ili kumpa uelewa mpana wa kulizungumza jambo lililomfika mwanasiasa na mwanaharakati huyo.

Sheikh Ponda anasema, Lissu aliniambia hivi: “Wewe (Sheikh Ponda), ulipingwa risasi na ukapelekwa gerezani na kidonda kinachululiza damu. Mimi nimeshambuliwa kwa makumi ya risasi. Damu nyingi imemwagika. Lakini nakuahidi sheikh wangu, damu yetu haitamwagika bure. Bali, itakuwa chachu ya ushindi.”

Ameongeza, “Lissu amehimiza mshikamano na alionyesha ana matumaini na Watanzania kwa harakati wanazozifanya. Tunamuombea arudi nchini kuendelea na majukumu yake.”

Kwa takribani miaka 25 sasa, Sheikh Ponda amekuwa akifahamika kama mwanaharakati wa kutetea “haki za waislamu.”

Alianza mapambano hayo, mwaka 1993 alipounda taasisi yake, akijikita katika kuita serikali iwachukulie hatua watuhumiwa wa mauwaji yaliyotokea kwenye Msikiti wa Mwembechai jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba zake kaadhaa, Sheikh Ponda amwekuwa akifanya marejeo katika historia ya nchi kabla na baada ya uhuru.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Rais mstaafu Mwinyi afariki dunia

Spread the loveRais Mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ally Hassan...

Habari za Siasa

Waziri mkuu Ethiopia atua Tanzania

Spread the loveWaziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia,...

Habari za Siasa

Babu Owino: Vijana msibaki nyuma

Spread the loveMbunge wa Embakasi Mashariki nchini Kenya, Paul Ongili Owino maarafu...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia: Hatutazuia watu kuingia barabarani

Spread the loveRAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itaendelea kuruhusu vyama...

error: Content is protected !!