April 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sakata la Uamsho moto; Masheikh wamvaa JPM, Kikwete, Bunge

Sheikh Issa Ponda Issa, Katibu ya Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania (picha kubwa). Picha ndogo, Rais John Magufuli

Spread the love

JUMUIYA na Taasisi za Kiislam nchini, imeibua upya sakata la masheikh wa Uamsho, waliopo mahabusu kwa takriban miaka sita sasa kwa madai ya kutokamilika ushahidi. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Katika Baraza la Eid lililoandaliwa na taasisi hiyo tarehe 5 Juni 2019 na kufanyika katika Msikiti wa Mtambani, jijini Dar es Salaam, taasisi hiyo imeeleza kuchukua mwelekeo mpya ili kusaidia viongozi hao wa dini waliokamatwa mwaka 2016, kwa madai ya kuhifadhi magaidi visiwani Zanzibar.

Viongozi wa taasisi hiyo, wameamua kumwandikia barua Rais John Magufuli; Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, Rais wa Zanzibar, Dk. Alli Mohammed Shein, Bunge la Jamhuri na wabunge mmoja mmoja wakieleza manung’uniko ya kuminywa haki viongozi hao.

Akisoma waraka ulioandaliwa na taasisi hiyo mbele ya waumini waliohudhuria Baraza la Eid Mtambani, Sheikh Ponda Issa Ponda, katibu wa jumuija hiyo ameeleza kuwa, taifa limeingia kwenye historia hai ya kuminya uhuru na haki kwa viongozi.

Kiongozi huyo amesema, suala la viongozi hao wa Uamsho waliokamatwa akiwemo Sheikh Farid Had Ahmad, Jamal Swalehe, Mselem Ali Mselemu, Nassor Abdallah, Hassan Suleiman, linaiabisha nchi hususan katika mfumo wa utoaji haki kutokana na kushindwa kuendesha kesi kwa kilichodaiwa kutokamilika kwa upelelezi.

Akisoma waraka huo uliopewa jina la ‘Kukandamizwa Haki za Masheikh Waliowekwa Gerezani kwa Miaka Sita Sasa’ Sheikh Ponda amesema, ni wakati sasa haki ikasimama kwa viongozi hao wa dini.

Amesema kuwa, kwa muda ambao masheikh hao wanasota gerezani bila kupatikana kwa ushahidi kwa miaka sita, kunawaumiza waumini wa dini hiyo sambamba na Watanzania wote wanaopenda haki pia na familia zao.

Akisoma barua maalumu aliyoielekeza kwa Rais Magufuli amesema kuwa, sasa ni wakati wa rais huyo anayejitanabaisha anaguswa pale anapoona watu wanadhulumiwa.

“Mheshimiwa rais, tumaini letu bila shaka unafahamu kadhia wapatao masheikh hao waliowekwa na serikali gerezani kwa miaka sita sasa pamoja na mamia ya waumini wao.

“Masheikh hao wamewekwa ndani kwa tuhuma za kumhifadhi gaidi, …kwa miaka sita sasa imeshindikana kupatikana kwa ushahidi, hivyo upelelezi haujakamilika ili kutoa nafasi ya usikilizwaji,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.

Amesema kuwa, masheikh hao wanasoteshwa magereza ilhali hawakufanya matendo yoyote ya ugaidi, isipokuwa kwa madai ya kuwapa hifadhi watu wanaodaiwa ni magaidi ambao wametajwa kuwa ni Sadic Absolom na Farah Omari.

Katika waraka huo amesema kuwa, ni wazi watu hao wakati masheikh wanadaiwa kuwa kuwafadhili watu hao walikuwa mahabusu huko unguja kwa tuhuma nyingine kwenye serikali ya Zanzibar.

Sheikh Ponda amesema kuwa, alihudhuria Siku ya Sheria Tanzania ya Mwaka 2017 na kuwa, Rais Magufuli alikuwa mgeni rasmi pia Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ambapo (Prof. Juma) alieleza mkakati wa mahakama kushughulikia kesi za muda mrefu.

“Wengi tuliokuwepo tulimuelewa kuwa kesi ya Masheik na Waumini hao haikuingizwa katika Mkakati huo.

“Mheshimiwa Rais kitendo cha upande wa Jamhuri kushindwa kukamilisha upelelezi wa shauri hili kwa miaka sita, na mahakama kushindwa kuendesha kesi hiyo ni wazi kwamba, vyombo hivi vinaharibu sifa ya nchi na misingi ya utolewaji haki katika mahakama zetu.” Imeeleza sehemu ya waraka huo.

Sheikh Ponda kwenye barua yake amemueleza rais kuwa, viongozi hao wa dini ni watu muhimu kwenye jamii yao kama walivyo viongozi wengine  na kwamba, kuwaumiza wao ni kuumiza umma na watu walio nyuma yao.

“Tunaamini unanafasi mzuri ya kuwajua na  sifa zao katika jamii hawana historia yoyote ya uhalifu waliyonayo na katika ukweli huu jamhuri imeshindwa kupata chochote cha kuwasaidia katika tuhuma zidi yao kama ushahidi.”

Katika waraka huo amemshauri Rais kurejea suala hilo kwenye mkondo wa sheria ili haki itendeke ilhali masheikh hao washafungwa jela kwa miaka sita. “Jamii inaamini kwa mamlaka uliyonayo unaweza kusitisha kigungo hiko.”

Amemuomba rais kujielekeza kwenye waraka uliyoondoa utata wa suala hilo uliyoandikwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Zanzibar, Othman Masudi mwaka 2013 kuhusu shauri hili.

Sheikh Ponda akinukuu sehemu ya Waraka huo amesema Mwanasheria Masudi alimshauri Rais wa Zanzibar kwa wakati huo juu ya shauri lile kushughulikiwa Zanzibar kutokana na kuwa na Mamlaka kamili juu ya kusikiliza mashauri yake na kwamba suala hilo sio la kimuungano.

error: Content is protected !!