January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Ponda amvaa Alhad Uchaguzi Z’bar

Spread the love

MGOGORO kuhusu kurudiwa kwa uchaguzi viswani Zanzibar unazidi kupasua nchi, sasa viongozi wa Dini ya Kiislam wametofautiana. Anaandika Faki Sosi.

Ikiwa ni siku moja baada ya Alhad Mussa Salum ambaye ni Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam kuunga mkono Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC) kutangaza tarehe ya uchaguzi visiwani humo, Jumuiya ya Taasisi za Kiislam Tanzania imepinga.

Sheikh Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini katika mkutano wake na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam amesema, kuruhusu kurudiwa kwa uchaguzi visiwani humo ni kupandikiza mbegu za chuki kwa wananchi.

Sheikh Ponda amesema kuwa uchaguzi uliofanyika Oktoba mwaka jana haukuwa na mashaka kwa kuwa, waangalizi wa nje pia walithibitisha hilo.

“Ripoti za waangalizi wa ndani na nje zilithibitisha kuwa uchaguzi haukuwa na dosari. Kuna sababu gani ya kurudia uchaguzi,” amehoji Sheikh Ponda.

Wakati Sheikh Ponda akihoji sababu za ZEC kurudiwa kwa uchaguzi huo, Sheikh Alhad aliipongeza tume hiyo na kuongeza “tunaiomba ZEC kusimamia kazi hii kwa haki, uadilifu na umakini mkubwa…”

Sheikh Alhad amesema kuwa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA) linaunga mkono uamuzi wa ZEC kurudia uchaguzi huku akikitaka Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kimesusia uchaguzi huo pamoja na vyama vingine kushiriki.

CUF kwenye mkutano wake wa Baraza Kuu la Uongozi uliofanyika tarehe 27 na 28 Januari mwaka huu kimetoa msimamo wa kususia uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu kwa kusema kuwa, hakuna sababu yoyote kwa chama hicho kushiriki. ZEC ilifuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba mwaka jana.

Hata hivyo, Sheikh Ponda amesema kuwa, ZEC haikuwa na sababu ya kufuta uchaguzi kutokana na ukweli kwamba, baada ya tume hiyo kutangaza matokeo, haina mamlaka ya kufuta.

Pamoja na kupinga kurudiwa kwa uchaguzi, Sheikh Ponda amehoji kuwa Sheikh Alhad amepata wapi kauli ya Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki), Sheikh Farid Hadi Ahmed kuwa anaunga mkutano marudio ya uchaguzi Zanzibar.

Sheikh Alhad kwenye mkutano wake jana alisema “Hata Amir wa Uamsho, Sheikh Farid Ahmed, pia anaunga mkono suala la kufanyika uchaguzi wa marudio kwa mujibu wa barua yake aliyonitumia mimi kutoka gerezani.”

Sheikh Ponda ameeleza kwamba, Sheikh Farid hawezi kutoa kauli hiyo na kwamba kama Sheikh Alhad anayo barua hiyo, aitoe hadharani.

“Sio jambo rahisi kuamini kwamba Sheikh Farid anaweza kutoa kauli hiyo, sio jambo rahisi kabisa na kama ni kweli basi atoe ushahidi wake,” ameeleza Sheikh Ponda.

Pia Sheikh Ponda ameonesha kushangazwa na ZEC kufuta uchaguzi wa rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani wa Zanzibar wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC imehalalisha na kutangaza matokeo ya Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania na Wabunge wa Bunge la Muungano ambao mfumo wake wa uchaguzi ni ule ule mmoja.

Shekh Ponda amesema kuwa uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake bado ni halali na kuongeza “sisi kama Taasisi ya Waislamu tunapinga kurudiwa kwa uchaguzi wa Zanzibar.”

Amesema kuwa, taasisi hiyo imeunga mkono hatua za mwanzo zilizochukuliwa na CUF pia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kunusuru hali ya kisiasa visiwani humo na kutaka majadiliano yaendelee.

Shekh Ponda amemshauri Rais John Magufuli kutimiza ahadi yake aliyoitoa bungeni ya kushughulikia mzozo huo kwa kushirikiana na Maalim Seif Shariff Hamad na Dk. Ali Mohammed Shein badala ya kkwepa kwa visingizio vilivyo halali.

Amesema kuwa, Rais Magufuli hajatoa tamko lolote na kwamba hajaeleza amefikia wapi katika kutimiza ahadi yake hiyo.

Sheikh Ponda ameonya kwamba vinaonekana viashiria vya kuvunjika kwa amani Zanzibar kutokana na CCM kuporwa haki za wananchi wa Zanzibar waliopiga kura kwa amani tarehe 25 mwaka jana na kumchagua Maalim Seif kuwa rais wa Zanzibar.

error: Content is protected !!