August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Ponda ‘amtumbua’ Rais Magufuli

Spread the love

SHEIKH Ponda Issa Ponda, Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, amekosoa utendaji wa Rais John Magufuli, hasa dhana ya kutumbua majipu, akisema ina kasoro za kiutawala, anaandika Happiness Lidwino.

Akizungumza na Mwanahalisi Online leo, Sheikh Ponda amesema utendaji wa Rais Magufuli ni wa kulipualipua.

“Ni kweli kwenye serikali kulikuwa na matatizo mengi, lakini lazima utaratibu kamili wa kuchukulia watu hatua ufuatwe,” amesema na kuongeza:

“Huwezi kuchukulia hatua watu bila kuwa na ripoti ya kitaalamu. Huko ni kufanya kazi kwa kulipuka. Watanzania watafurahi zaidi kama serikali haitaingia hasara kutokana na kazi hiyo iliyo na shaka katika utekelezaji wake.”

Amesema ingekuwa bora kwa Rais Magufuli kusubiri ripoti za wataalamu wake, na si ‘kutumbua majipu’ kabla ya kupata ripoti. Anasisitiza, “jambo hili halipo sawa hata kidogo.”

Anasema dhamira ya kurejesha nidhamu serikalini ni nzuri na inahitajika sana, lakini namna ya utekelezaji wa dhamira yake hakuuanza vizuri.

“Juzi Rais Magufuli amepokea ripoti kutoka kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Angepaswa kuanza kuifanyia kazi ripoti hiyo ili kuepuka madhara kama yale ya kukamata meli ya uvuvi kwenye Pwani ya Dar es Salaam mwishowe serikali ikaingia gharama,” amesema Sheikh Ponda.

error: Content is protected !!