May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Ponda adaiwa kuvamiwa

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam, Sheikh Ponda Issa Ponda

Spread the love

 

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda, anadaiwa kuvamiwa na mtu asiyejulikana, ofisini kwake katika Msikiti wa Bungoni, uliopo Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).

Kwa mujibu wa taarifa ya mlinzi wa Sheikh Ponda, Jamali Shekitundu, tukio hilo limetokea asubuhi ya leo Jumatano, tarehe 9 Juni 2021, baada ya kuwasili ofisini kwake.

Taarifa ya Shekitundu imesema, baada ya Sheikh Ponda kushuka katika gari lake, kuelekea ofisini kwake, mwanamke mmoja aliyekuwa na mtoto, alimsimamisha na kumuomba hela, lakini kiongozi huyo wa kidini alimjibu hana.

Inadaiwa kuwa, baada ya mwanamke huyo kukosa pesa, alianza kumshambulia Sheikh Ponda kwa kumpiga makonde, hali iliyomfanya akimbie eneo la tukio, kuelekea ofisini kwake.

Taarifa hiyo imedai kuwa, baada ya Sheikh Ponda kukimbilia ofisini kwake, mwanamke huyo alianza kushambulia kwa mawe gari yake aina ya BMW X5.

Gari la Shekhe Ponda Issa Ponda lilopasuliwa wakati wa uvamizi huo

“Akiwa ghorofani Sheikh Ponda alisikia kishindo upande liliko egeshwa gari lake, alipochungulia alimuona mtu huyo akivunja kwa kutumia matofali yaliyokuwepo jirani ya eneo hilo,” imesema taarifa ya Shekitundu.

Taarifa ya Shekitundu imesema, baada ya mwanamke huyo kuanzisha vurugu hizo, majirani walimkamata na kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Pangani wilayani Ilala.

“Polisi wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya walichukua maelezo ya Sheikh Ponda pamoja na yake, kisha wakarudi kituoni,”

“Walipokuwa kituoni, mtu huyo alitoroka kwa ufundi mkubwa ambapo Polisi walichukua hatua za haraka za kumsaka na hatimaye kumtia mbaroni akiwa amefika umbali wa nusu kilometa, jirani ya ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, iliyoko Boma,” imesema taarifa ya Shekitundu.

MwanaHALISI Online imemtafuta Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Debora Magiligimba, kwa ajili ya ufafanuzi kuhusu tukio hilo, ambaye amesema hajapata taarifa zake.

Aidha, Kamanda Magiligimba amesema anafuatilia undani wa tukio hilo, kisha atatoa taarifa baadae.

error: Content is protected !!