January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Sheikh Kishki aundiwa kiroja mtandaoni

Spread the love

ULAMAA maarufu wa Kiislamu nchini, Sheikh Nurdin Kishki, amesingiziwa taarifa zisizo na msingi na watu waliofungua akaunti katika mtandao wa kijamii wa Facebook na kuandika taarifa zinazomuonesha kama swahiba wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda. Anaandika Jabir Idrissa … (endelea).

Sheikh Kishki ambaye ni mhadhiri kipenzi kikubwa cha Waislam nchini na kote Afrika Mashariki, amefika studio za kituo cha televisheni cha Azam Tv usiku huu, na kukanusha kumiliki akaunti ya aina hiyo.

Amesema hana akaunti katika mtandao wowote wa kijamii, na kuongeza uzito wa kauli akisema, “sijui kabisa, wala sijihusishi na mambo haya ya kupenda mitandao.”

Sheikh Kishki amesema anaamini waliofanya hivyo ni adui zake kwa sababu anasema ni kawaida ya binaadamu kutokuwa kipenzi cha kila mtu, na pale inapotokea maamuzi, adui hufanya atakacho cha kumchafua anayemchukia.

Hakumtaja mtu yeyote anayedhani ametengeneza akaunti hiyo na kuipa jina lake, lakini amesema kuwa kitendo hicho kilifanywa Agosti 13 wakati akiwa nje ya nchi kwa ziara za shughuli zake za kidini.

“Sikuwepo nchini, lakini wenzangu wamenipa taarifa za jambo hili nikashtuka kwa sababu si mambo yangu kuhangaikia mitandao,” amesema na kwamba aliporudi aliharakia kwenda Kituo cha Polisi Chang’ombe, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam, anakoishi na kutoa taarifa.

Sheikh Kishki ambaye alizaliwa Agosti 18 mwaka 1986, amesema ameshangazwa na kitendo hicho kiovu na kuomba serikali ishughulike kudhibiti waovu kama hao.

Kuhusu kama ana uhusiano na Waziri Mkuu Pinda, amesema hayuko karibu na kiongozi huyo na anasikitika kuoneshwa kuwa ana ukaribu naye na anatoa maneno ya uchochezi.

error: Content is protected !!