March 5, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shamba la Rais Kikwete lavamiwa

Rais Jakaya Kikwete na Mama Salma akiwa shambani

Spread the love

MBUNGE wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema shamba la baba yake, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete lililoko kata ya Kibindu wilayani Bagamoyo mkoa wa Pwani, lilivamiwa na mfugaji mwenye ng’ombe wasiopungua 800. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Ridhiwani ameyasema hayo leo tarehe 26 Oktoba 2018 mbele ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu wakati akizungumzia kuhusu changamoto ya uvamizi wa maeneo unaofanywa na baadhi ya wafugaji wa kuhama hama, katika mkutano wa hadhara uliofanyika jimboni kwake, Chalinze.

Akielezea kuhusu tukio hilo, Ridhiwani amesema amebaini uvamizi huo baada ya kwenda shambani huko na Afisa Polisi wa Chalinze wiki tatu zilizopita, na kumkuta mfugaji huyo anayetokea mkoani Manyara, akilisha ng’ombe hao.

“Mfano mmoja ulio hai, wiki tatu zilizopita kamanda wangu wa polisi wa hapa Chalinze nilikwenda nae Kibindu, na ili kujua hii hali imekuwa mbaya kuna mfugaji mmoja kutoka Manyara amekwenda kuvamia shamba la rais mstaafu, amekwenda kuweka ndani ng’ombe wasiopungua 800, kama sio elfu moja na anasema kabisa kwamba kama hajalisha pale akalishe wapi,” amesema na kuongeza Ridhiwani.

“Wakati mwingine sisi kwa nafasi zetu kama wabunge tunaogopa hata kutumia nguvu kwa sababu zile mali nyingine ni mali binafsi, ninaamini haya yanaweza kutatuka kama wizara yetu ya kilimo mifugo itaweka mguu.”

Akizungumzia kuhusu changamoto hiyo, Mama Samia amesema serikali itafanyia kazi suala hilo ili kuhakikisha wafugaji wanaofuga kwa kuhama hama hawavamii maeneo ya watu.

“Kwenye Suala la ufugaji wa kuhama hama na kuvamia maeneo, nashukuru sana aibu waziri mifugo na uvuvi amelitolea ufafanuzi mzuri, lakini niahidi serikali italisimamia,” amesema Mama Samia.

error: Content is protected !!