Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shaka: CCM hakuna mpasuko, Ndugai sio wa kwanza
Habari za SiasaTangulizi

Shaka: CCM hakuna mpasuko, Ndugai sio wa kwanza

Shaka Hamdu Shaka, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM
Spread the love

WAKATI Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisema ndani ya CCM kuna ‘homa ya urais’ kuelekea uchaguzi mkuu 2025, Katibu wa NEC- Itikadi  Uenezi CCM, Shaka Hamidu Shaka ameibuka na kusema hakuna mpasuko ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar … (endelea).

Tarehe 4 Januari mwaka huu akipokea taarifa ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19, Rais Samia alisema;

“Ni uhuru wa mtu kusema chochote, lakini inashangaza mtu anayetegemewa kushirikiana na Serikali kwenye safari ya maendeleo ‘kuargue’ kuhusu tozo na mkopo wa trilioni 1.3 kwa sababu taarifa zote za uchumi zinapita kwake, Ni homa (fever) ya 2025, wasameheni.”

Aidha, leo tarehe 9 Januari Shaka amesema ukifuatilia kitabu cha historia ya CCM kina matukio makubwa ya kusisimia na kwa nyakati zote CCM imekuwa ikipita kwenye mawimbi, dhoruba, mitikisiko lakini kamwe haijawahi kupasuka kwa sababu iko imara.

Amesema inawezekana suala la Ndugai kujiuzulu baadhi ya watu wakakitabiria CCM kuwa kutatokea mpasuko lakini hakuna kitu kama hicho.

Shaka alienda mbali na kutolea mfano mwaka mtikisiko wa mwaka 1984 ambao amesema kama ni mpasuko ungetokea wakati huo.

“Mwaka 1984, kulitokea jambo kubwa la kihistoria, uliondoka muhimili mkubwa… aliondoka Rais wa Zanzibar, makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mjumbe wa kamati kuu, lakini mwaka huohuo likatokea jambo lingine kubwa wakati Rais Abood Jumbe Mwinyi anaondoka, Aliyekuwa waziri kiongozi Ramadhan Ali Fakhi naye aliondoka.

“Serikali wakati huo haikuwa na kiongozi wa aina yoyote lakini CCM ilibaki kuwa imara, ilibaki kuwa madhubuti.

“Lakini akapatikana Mzee Mwinyi majukumu yakaendelea. Kujiuzulu kwa Ndugai sio jambo la kwanza, Seif Sharif Hamadi na jopo lake, Seif alikuwa waziri kiongozi, mkuu wa idara za CCM akiwa na wenzake saba ‘heavy weight’ waliondoka na chama kilibaki imara.

“Ukienda kwenye mhimili wa Serikali ameondoka Mzee Mwinyi akiwa waziri wa mambo ya ndani, Mzee Lowassa akiwa waziri mkuu wa Tanzania kwa hiyo kitabu cha historia ya CCM kina matukio ambayo ukitazama kwa haraka unaweza kusema CCM imemalizika lakini kwa CCM kumalizika kwa jambo moja ni kuja kwa nguvu mpya kujipanga na kwenda kwa nguvu zaidi,” amesema.

Amesema hayo yote yamefanyika wakati huo ambapo demokrasia ilikuwa haijakomaa kama sasa ndio maana CCM inatangaza nafasi hiyo ya kujaza Spika wa Bunge kwa kujiamini.

Spika Job Ndugai

“Kwamba atapatikana mwana CCM mzuri kabisa kwa sababu lazima tufahamu kuwa CCM ni chama ambacho hakina uhaba wa viongozi, ndani yake viongozi wameandaliwa, wamepikwa, mtawaona muda utakapofika… kumesheheni viongozi na huu ndio uimara wa chama chetu,” amesema.

Amesema kama chama hicho kingekuwa dhaifu kingekuwa kinapata taabu kwamba akiondoka kiongozi nani atajaza nafasi yake.

“Mfano mzuri tunao tumepata mtihani, Mama Samia amepanda anayofanya leo ni mambo makubwa ya kupigiwa mfano ameliletea Taifa letu heshima. Siku zote CCM haifanyi mambo yake kwa kubahatisha.

“Hakuna chama ambacho kimekomaa kama CCM na wala haina hofu kwamba labda mtu ameanzisha makundi, vuguvugu kwa sababu misingi katiba, taratibu, kanuni na miongozo ya chama iko wazi kabisa,” amesema.

Amesema kamwe hawatochukua bakora kuwachapa walioanzisha makundi kwa sababu taratibu zipo lakini pia chama kina utamaduni ambao kitaendelea kuuheshimu.

“Katika hili niwaombe wale wenye sifa muda utakapo wajitokeze kwa wingi kuomba nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya shina, tawi, jimbo, kata, mkoa hadi taifa. Kila mwanachama mwenye sifa ajitokeze kuomba.

“Wasiwe na hofu kama Rais Samia alivyosema kwamba kitakachoangaliwa ni sifa na vigezo ili uweze kupata nafasi ndani ya chama lakini hataonewa mtu wala kuminywa, tutaheshima msingi wetu, wa utu wa mtu na maelekezo ya katiba yetu kwamba kila mtu ana haki ya kuchagua na kuchaguliwa,” amesema.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!