Wednesday , 24 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shahidi wa Serikali adai hakuona kina Mbowe wakipanga uhalifu
Habari za SiasaTangulizi

Shahidi wa Serikali adai hakuona kina Mbowe wakipanga uhalifu

Spread the love

 

SHAHIDI wa Jamhuri, Innocent Ndowo (37) ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi nchini Tanzania kuwa, uchunguzi alioufanya wa mawasiliano ya simu ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, hakuona kiashiria chochote cha kupanga vitendo vya uhalifu. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea). 

Ndowo ambaye ni Askari wa Jeshi la Polisi akiwa shahidi wa kumi, amesema hayo jana Jumatano, tarehe 19 Januari 2022, mbele ya Jaji Joachim Tiganga wakati akitoa ushahidi wake, jijini Dar es Salaam.

Ni katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu, Adam Kasekwa, Halfan Mbwire na Mohamed Ling’wenya ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).

Ndowo ambaye ni mchunguzi wa kisayansi mwenye uwezo wa kuingilia mawasiliano ya simu, alieleza alichokiona alipokuwa akihojiwa na kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala.

Shahidi huyo alisema, Julai 2021 alifanya uchunguzi wa mawasiliano baina ya Mbowe na Dennis Urio ya njia ya Telegram, WhatsApp, meseji ‘sms’ katika simu nane alizopelekewa na simu nne zilionesha matokeo chanya huku nne hazikuonesha.

Kwa mujibu wa Ndowo, Mbowe anadaiwa kuwasiliana na Denis Urio, anayedaiwa kumpa kazi ya kuwatafuta waliokuwa makomandoo hao wa JWTZ kwa lengo la kupanga njama za ugaidi.

Mahojiano ya Kibatala na Ndowo ambaye amepata mafunzo ya eneo hilo analofanyia kazi ndani na nje ya Tanzania yalikuwa hivi;

Kibatala: Kwa mujibu wa barua iliyotoka ofisi ya DCI ambayo haipo, hizo namba na simu zinachunguzwa kwa tuhuma za ugaidi?

Shahidi: Nimeona kosa limeandikwa pale

Kibatala: Mwambie Jaji tuhuma za ugaidi ni subject ya uchunguzi wako?

Shahidi: Barua ile imetaja jalada namba na kosa la tuhuma za ugaidi

Kibatala: Ulifanya basic detective course kama train? Ulifanya mafunzo yote ya kijeshi ikiwemo upelelezi?

Shahidi: Ni yapi? Mengine siwezi kueleza

Kibatala: Sehemu ya mafunzo ni upelelezi au la?

Shahidi: Baadhi ya watu wanafundishwa upelelezi

Kibatala: Wewe? Ulifundishwa basics za upelelezi?

Shahidi: Nilisoma basics za upelelezi

Kibatala: Barua inasema kosa la kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, achana na terms of reference (hadidu rejea) mwambie Jaji katika  uchunguzi wako wa vifaa, kwa mujibu wako unaweza chunguza kosa ukaona kosa A na kosa B?

Mwambie jaji kipi uliona kinakupa kiashiria watu walipanga njama za vitendo vya ugaidi?

Shahidi: Swali hilo anapaswa kujibu mpelelezi

Kibatala: Nasema wewe

Shahidi: Mimi nilifanya analysis, mimi sikujua kitu gani kinahusisha tuhuma za ugaidi

Kibatala: Extraction (unyonyaji taarifa kutoka katika simu) yako Iliona kiashiria chochote cha watu kupanga njama  za ugaidi?

Shahidi: Nilichokiona ndicho nilichokitoa

Kibatala: Katika uchunguzi wako ukiacha term of reference, uliona mawasiliano ya watu wanapanga au wanamtaja Sabaya?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji,  katika terms of reference haikumtaja Sabaya, record ingeelekeza kumtafuta Sabaya ningechunguza

Kibatala: Ni wewe ama sio wewe dakika chache zilizopita ulisema unaweza ukapata reference kuhusu kosa A, ukaona na B?

Shahidi: Nilisema unaweza kuta vitu vingine, issue zingine ukaunganisha pamoja na hiyo issue

Kibatala: Hivyo vitu ulivyoviona kuna mahala uliona mawasiliano kutoka hizo simu nane, watu wakipanga kufanya chochote cha kumdhuru Sabaya?

Shahidi: Sikuelekezwa kufanya uchunguzi kuhusu Sabaya. Ningekuwa nimeombwa kutafuta ningefanya,  lakini sikuombwa kutafuta

Kibatala: Tukiachana na  terms of reference kuhusu Sabaya, umeona kuhusu watu kulipua madaraja katika ushahidi wako wote uliowahi ona. Umesema  chochote kinachohusiana na watu kupanga njama za ugaidi?

Shahidi: Nilichokiona ndicho nilichokitoa mahakakani

Kibatala: Wakati unafanya extraction  kuna mahala popote uliona mawasiliano ambayo yanaonesha watu wamefanya maandamano nchi nzima?

Shahidi: Sikuelekezwa kufanya uchunguzi huo

Kibatala: Uliona mahala popote watu wakizungumza chochote kuhusu kupeana, kuiba au kununua bunduki aina ya Rugger A 5340?

Shahidi: Naomba urudie

Kibatala: Katika process yote uliwahi ona mawasiliano, yawe Telegram ambayo watu wenye navyo wakizungumzia bunduki yenye usajili namba A5340 aina ya Rugger?

Shahidi: Unaongea kitu ambacho sikufanyia kazi, sikuombwa kutafuta hiko kitu

Kibatala: Kuna sms Telegram  au WhatsApp inaonesha nimetuma fedha kwa ajili ya kufanya ugaidi?

Shahidi: Nakumbuka text katika  Telegram kuna mawasiliano ya fedha

Kibatala: Nitafutie sehemu ambayo meseji ambazo  umezi-extract inasema  kwamba fedha hizi ni kwa ajili ya kufanya vitendo vya kigaidi, iko meseji?

Shahidi: Mheshimiwa Jaji naomba ajikite kwenye taarifa nilizofanyia kazi, kilichopo pale ndicho nilichokifanya

Kibatala: Kwa uchunguzi wako wewe ungekuta taarifa za kupanga uhalifu ungeacha kuandika kwenye riport yako kwa sababu hujaambiwa kwenye _terms of reference?_

Shahidi: Mimi ni askari polisi, kama ningekuta meseji za kupanga uhalifu ningeweka kwenye ripoti yangu.

Katika kesi hiyo, Mbowe na wenzake wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo la kukutwa na silaha aina ya Rugger, kukutwa na sare na vifaa vya JWTZ na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Pia, kushiriki vikao vya kupanga njama za ugaidi, kutoa fedha zaidi ya Sh.600,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo na kupanga kulipua vituo vya mafuta na maeneo yenye mikusanyiko ya watu.

Shtaka lingine ni la kutaka kushuru viongozi wa Serikali, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya ambaye sasa ni mfungwa anayetumikia adhabu yake Gereza la Kisongo mkoani Arusha.

Jaji Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi leo Alhamisi, tarehe 20 Januari 2022, ambapo mawakili wa Jamhuri wataendelea kumuuliza maswali ya ufafanuzi kuhusu ushahidi wake alioutoa wakati wa maswali ya dodoso aliyoulizwa na upande wa utetezi.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

Habari za Siasa

Serikali kuanzisha mradi wa Gridi ya maji ya Taifa

Spread the loveWaziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika mwaka wa fedha...

error: Content is protected !!