May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi wa Jamhuri: Mbowe, wenzake sikuwakuta na mabomu, vilipuzi wala mafuta ya petroli

Spread the love

 

MPELELEZI wa Makosa ya Jinai katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Goodluck Minja, amedai washtakiwa wawili katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, hawakukutwa na mabomu, vilipuzi na au mafuta ya petroli, walipokamatwa mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Goodluck ametoa madai hayo leo Ijumaa, tarehe 21 Januari 2022, akiulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Utetezi, John Mallya, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Jinai, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Ni baada ya shahidi huyo wa 11 wa Jamhuri, kueleza namna alivyoshiriki zoezi la kuwakamata washtakiwa hao, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro, tarehe 5 Agosti 2020.

Ambapo alidai, Kasekwa na Ling’wenya walikutwa na kete za dawa zidhaniwazo kuwa za kulevya na simu. Kasekwa anadaiwa kukutwa na Bastola yenye namba za usajili A5340 aina ya Rugger.

Mbowe na wenzake waliokuwa Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Ling’wenya, Kasekwa na Halfan Bwire Hassan, wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, ikiwemo kupanga njama za kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu, maeneo mbalimbali nchini. Wanadaiwa kupanga njama hiz kati ya Julai na Agosti 2020.

Wakili Mallya alimhoji Goodluck kama ifuatavyo;

Mallya: Ulivyowakamata watuhumiwa mliwakuta na petroli au kidumu wamekaa nacho?

Shahidi: Hapana

Mallya: Bomu la kulipua?

Shahidi: Hapana

Mallya: Mashine ya kulaza magogo barabarani?

Shahidi: Hapana

Wakati huo huo, Goodluck alidai hafahamu mpelelezi wa kesi hiyo, ambapo mahojiano yao yalikuwa kama yafuatavyo;

Mallya: Mpelelezi wa kesi hii alikuwa nani?

Shahidi: Sijui ni nani

Mallya: Kwenye namba ya jalada kuna tuhuma ngapi unazofahamu shahidi?

Shahidi: Sifahamu, zaidi ya kula njama sifahamu

Baada ya kutoa ushahidi huo, Jaji Tiganga ameahirisha kesi hiyo hadi Jumatatu, tarehe 24 Januari 2022, ambapo Goodluck ataendelea kuulizwa maswali ya dodoso na mawakili wa utetezi.

error: Content is protected !!