October 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi wa Jamhuri: Chadema hawakubeba silaha

Spread the love

SHAHIDI namba sita wa Jamhuri, Koplo Charles katika kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi waandamizi wa Chadema, ameeleza kutoona wafuasi wa chama hicho wakiwa na silaha. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akitoa ushahidi wake tarehe 21 Agosti 2019 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu jijini Dar es Salaam, Thomas Simba shahidi huyo ameeleza kuwa,wakati akirekodi picha za video aliyoipa mahakama kama ushahidi, hakuona wafuasi wa Chadema wakiwa na silaha.

Kesi hiyo ya uchochezi namba 112/2018, inawakabili viongozi wa Chadema, miongoni mwao ni Freeman Mbowe, mwenyekiti wa chama hicho Taifa; Dk. Vincent Mashinji, Katibu Mkuu; John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara na Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Akitoa ushahidi wake mahakama hapo Koplo Charles amedai, hakuona wafuasi wa chama hicho wakiwashambulia askari polisi.

Ni wakati ambao alikuwa akirekodi picha za video katika mkutano wa kufunga kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni, tarehe 16 Februari 2018 katika uwanja wa Buibui, jijini Dar es Salaam.

Koplo Charles alitoa ushahidi huo wakati akiulizwa maswali na wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala. Hata hivyo, Koplo Charles ameieleza mahakama kuwa, video aliyorekodi haioneshi tarehe ya kurekodiwa.

Kwenye kesi hiyo upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Wakuu, Faraja Nchimbi, Dk. Zainabu Mango, Wakili wa Serikali Mwandamizi Wankyo Simon na Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantori.

Upande wa utetezi Wakili Kibatala alisaidiwa na Jeremia Mtobesya, Hekima Mwasipu na Fredy Kiwelo. Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo mpaka leo tarehe 21 Agosti 2019.

error: Content is protected !!