Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shahidi wa Jamhuri aeleza walivyowazuia wenzake Mbowe kufanya ugaidi
Habari za SiasaTangulizi

Shahidi wa Jamhuri aeleza walivyowazuia wenzake Mbowe kufanya ugaidi

Spread the love

 

MPELELEZI wa Makosa ya Jinai katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha, Askari Polisi namba H4347 Goodluck, amedai Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Arusha, ACP Ramadhan Kingai, aliunda timu maalum kwa ajili ya kudhibiti kikundi kilichoundwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, kufanya vitendo vya ugaidi nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Goodluck ametoa madai hayo leo Ijumaa, tarehe 21 Januari 2022, akitoa ushahidi wake katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake, kwenye Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Shahidi huyo wa 11 wa Jamhuri, akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, amedai timu hiyo ilianza kazi ya kudhibiti kikundi hicho tarehe 5 Agosti 2020, baada ya kuwakamata watuhumiwa wawili, Ling’wenya na Kasekwa, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Yafuatayo ni mahojiano kati ya Wakili Hilla na Goodluck;

Hilla: Baada ya Afande Kingai kupewa maelekezo ya kuunda timu ya kufanya kazi maalumu, jambo gani alieleza?

Shahidi: Alisema amepata taarifa kuna kikundi cha watu wamepanga njama za kutenda ugaidi hapa nchini, katika maeneo mbalimbali.

Hilla: Aliwaeleza kitu gani kingine?

Shahidi: Alituambia kwa taarifa alizopata kuna watu wengine wako Kilimanjaro, Moshi na akatuambia kikundi hicho wamepanga kuwadhuru viongozi, akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Hai, wamepanga kuhamasisha maandamano nchini yasiyokuwa ya kikomo.

Pia alitueleza kikundi hicho kimeratibiwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Freeman Mbowe.

Afande Kingai alitueleza kwamba, kikundi hicho kimepanga kuchoma vituo vya mafuta, kukata miti na magogo kupanga barabarani nchini, ili kuleta taharuki kwa wananchi nchi ionekane haitawaliki.

Afande Kingai alituambia kwamba, taarifa alizo nazo kuna wahalifu wengine wako Moshi, kwa hivyo twende Moshi kuzuia uhalifu huo usifanyike.

Hilla: Kuzuia uhalifu kwa namna gani?

Shahidi: Afande Kingai alituambia tukawakamate watuhumiwa hao.

Hilla: Na kitu gani kingine tena kilifanyika?

Shahidi: Baada ya kutoa taarifa hiyo na maelekezo tuliondoka kituoni kueleka Moshi.

Hilla: Ieleze mahakama safari ya kuelekea Moshi ilihusisha kina nani?

Shahidi: Ilihusisha Afande RCO Kingai, Jumanne, Mahita, Koplo Francis pamoja na PC Aziz, ambaye ni dereva.

Hilla: Baada ya kufika Moshi nini kilifanyika?

Shahidi: Tulienda maeneo ya Central Polisi Moshi.

Hilla: Mambo gani mliyafanya siku hiyo?

Shahidi: Kingai alishuka kwenye gari kufanya mawasiliano, baada ya hapo tukapanda gari kwenda Moshi Mjini ili kuwakamata wahalifu hao.

Hilla: Ielezee mahakama kazi yenu kwa siku hiyo ilikuwaje?

Shahidi: Kazi yetu kwa siku hiyo ilikuwa kuwatafuta wahalifu, lakini hatukufanikiwa kuwakamata.

Hilla: Unasema mlizunguka maeneo mbalimbali Moshi Mjini, mlifanya hivyo baada ya muda gani?

Shahidi: Tulifanya hivyo hadi muda wa saa tano usiku.

Hilla: Ilipofika muda huo nini kilifanyika?

Shahidi: Ilipofika saa 5 kuelekea saa 6 usiku, Afande alisema kwa kuwa hatujafanikiwa kuwakamata na anaendelea kupata taarifa za wahalifu walipo, alisema tukapumzike ili tuendelee na zoezi la kuwakamata wahalifu kesho yake.

Hilla: Kesho yake tarehe 5 Agosti 2020 umakumbuka siku hiyo mlianza na jambo gani?

Shahidi: Nakumbuka tarehe 5 Agosti baada ya kuamka asubuhi tulikuwa tunaendelea na ufuatiliaji, Afande Kingai alipokea taarifa kwa aliyekuwa anampa taarifa. Muda wa saa 7 mchana akapokea taarifa hawa watuhumwia wameonekana maeneo ya Rau Madukani.

Hilla: Baada ya taarifa hiyo Kingai alitoa maelekezo gani?

Shajidi: Amesema aliambiwa watu hao muonekano wao wamekaaje na wako maeneo ya Rau, akatuambia mmoja wao amevaa jezi ya Taifa Starts na koti jeusi.

Mwingine amevaa shati lenye rangi nyekundu na jaketi la kijani, mwingine shati lenye maua maua yenye rangi na suruali nyeusi, baada ya kutoa taarifa hiyo akatuongoza kwenda kwenye eneo la tukio.

Hilla: Kwa maana kwamba kulikuwa na watuhumiwa wangapi shahidi?

Shahidi: Kulikuwa na watuhumiwa watatu.

Hilla: Mmeshaelezwa walivyovaa, baada ya hatua hiyo kilichofuata ni nini?

Shahidi: Baada ya Kingai kutueleza hivyo tuliondoka kituoni tukaeleka maeneo ya Rau Madukani, kwenda kuwakamata pale.

Hilla: Sasa mmeshafika eneo la Rau Madukani, ifahamishe mahakama mlifanya kitu gani?

Shahidi: Baada ya kufika Rau tulipaki gari, Afande Kingai alimpa maelekezo Afande Mahita ashuke kwenye gari kuangalia hao watuhumiwa wamekaa wapi.

Hilla: Kufuatia maelekezo hayo nini kiliendelea?

Shahidi: Tulishuka kwenye gari tukaenda kufanya surveillance ya watuhumiwa.

Hilla: Shahidi ilezee mahakama kwamba ilichukua muda gani kwa Mahita kufanya tukio hilo?

Shahidi: Haikuchukua muda mrefu, Mahita alirudi akasema nimewaona watu watatu. Alitoa maelekezo tushuke kwenye gari tukakamate watuhumiwa, aligawa timu mbili.

Hilla: Ambazo ni zipi?

Shahidi: Moja alikuwa anaongoza Kingai, mimi na Jumanne, nyingine alikuwa Afande Mahita na Francis

Hilla: Mliskia kitu gani?

Shahidi: Nilisikia sauti ya Mahita akisema mko chini ya ulinzi

Hilla: Mlifanya nini?

Shahidi: Baada ya kusikia sauti tulielekea kwenye eneo la tukio, baada ya kufika tukawakamata, tukawaweka chini ya ulinzi.

Goodluck amedai kuwa, baada ya kuwakamata watuhumiwa hao, walifanyiwa upekuzi na kukutwa na kete za dawa zidhaniwazo kuwa za kulevya.

Aidha, Adam alikutwa na bastola yenye usajili wa A5340 aina ya Rugger, na simu.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbowe na wenzake, wanakabiliwa na mashtaka sita ya ugaidi, likiwemo la kutaka kudhuru viongozi wa Serikali, kulipua vituo vya mafuta na mikusanyiko ya watu wengi, kutoa fedha zaidi ya Sh. 600,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo hivyo.

Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Julai hadi Agosti 2020, katika maeneo ya mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

Habari za Siasa

CCM yakemea ufisadi, yaipa kibarua TAKUKURU

Spread the love  CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekemea vitendo vya ubadhirifu wa...

Habari za Siasa

Bajeti ya Ikulu 2024/25 kuongezeka, bunge laombwa kurudhia Sh. 1.1 trilioni

Spread the love  WIZARA ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa...

error: Content is protected !!