Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shahidi wa Jamhuri adai hajui kosa la mwenzake Mbowe
Habari za Siasa

Shahidi wa Jamhuri adai hajui kosa la mwenzake Mbowe

Spread the love

 

ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luten Denis Urio, amedai hafahamu kosa na sababu za kukamatwa kwa Halfan Bwire Hassan, mshtakiwa wa kwanza katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na kuwa waaaofahamu suala hilo ni wapelelezi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Luteni Urio ametoa madai hayo leo Alhamisi, tarehe 27 Januari 2022, akihojiwa maswali ya dodoso na Wakili wa Hassan, Nashon Nkungu, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumi Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Shahidi huyo wa 12 wa Jamhuri, ametoa madai hayo baada ya Wakili Nkungu kumuuliza kwa nini Hassan ameshtakiwa, wakati alifuata maagizo yake ya kumpa taarifa za mipango ya Mbowe kutaka kufanya vitendo vya ugaidi.

Wakili Nkungu alimhoji swali hilo, baada ya Luteni Urio jana kudai kuwa, alipowaunganisha makomando hao (washtakiwa) na Mbowe aliwapa maelekezo ya kumpa taarifa pindi watakapoona matukio ya kiuhalifu kwa mwanasiasa hao.

Lakini hawakufanya hivyo, ndipo tarehe 4 Agosti 2020, alimpigia simu Hassan, ambaye alimueleza walikengeuka kwa yale aliyowalekeza, kwani kazi ya ulinzi aliyowaeleza wanakwenda kufanya kwa Mbowe, ilibadilika kwa kuwa mwanasiasa huyo aliwashawishi kufanya kazi nyingine.

Ya kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro, kumshambulia aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya na kuwa kabla ya tarehe 7 Agosti 2020, wanatakiwa wawe wamekamilisha kazi hiyo.

Luteni Urio alidai kuwa, taarifa alizopewa na Hassan, alizifikisha kwa aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, ACP Ramadhan, aliyekuwa kiongozi wa timu iliyoundwa kumfuatilia Mbowe.

Hivyo taarifa hizo ziliwezesha Jeshi la Polisi kumkamata mshtakiwa wa pili (Kasekwa) na wa tatu (Ling’wenya), mkoani Kilimanjaro tarehe 5 Agosti 2020.

Mahojiano ya Wakili Nkungu na Luteni Urio yalikuwa kama ifuatavyo;

Nkungu: Kuna tukio la tarehe 4 Agosti 2020, Bwire alikupigia simu akakuambia shughuli imebadilika, sio uliotuambia tuje kufanya. Alikuambia aligundua hilo muda gani?

Shahidi: Alinipigia simu majira ya saa 2 asubuhi.

Nkungu: Huyu Bwire alikuwa anapata maelekezo yako ya kukupigia simu kwamba ukiona vitendo havieleweki unipigie simu, alikuwa anafuata maelekozo yako, ni sahihi?

Shahidi: Mimi ndiyo nilimpigia simu kwa mujibu wa maelezo yangu mimi, akaniambia mlichotuitia kimekengeuka.

Nkungu: Bwire alikuambia lini issue (suala) ilibadilika?

Shahidi: Yeye hakuniambia ni lini

Nkungu: Wewe ulisema Bwire amekuambia tarehe 4 kwa kukupigia simu, alifanya jambo sahihi au jema?

Shahidi: Lilikuwa jambo sahihi.

Nkungu: Kwa mujibu wako, taarifa za Bwire zilipelekea kesho yake tarehe 5 Agosti 2020 washtakiwa wa pili na wa tatu wakakamatwa Rau Madukani?

Shahidi: Ni sahihi.

Nkungu: Ulirudisha mrejesho kwa Kingai kwamba Bwire amenipatia information (taarifa), ulirudisha taarifa hizo?

Shahidi: Ni sahihi

Nkungu: Baada ya pale hata wewe ilikushangaza Bwire kukamatwa, si ndiyo?

Shahidi: Hapana sikushangaa

Nkungu: Kwani wewe kwa uelewa wako kwa mazingira hayo kosa la Bwire kwenye hii kesi yote liko wapi?

Shahidi: Sijui.

Nkungu: Hufahamu involvement (ushiriki) ya Bwire kwenye makosa haya ya kupanga njama za ugaidi?

Shahidi: Mimi siwezi nikafahamu, mimi sijui.

Nkungu: Wewe uko nje na Bwire informer (mtoa taarifa), wako yuko mahakamani ameshtakiwa na wewe uko nje ukiendelea kula maisha?

Shahidi: Sijui kwa nini, sijafahamu kwa nini amekamatwa, hao waliompeleleza wanajua walimkuta na kosa gani.

Nkungu: Kwani wewe una u-special gani au una mkataba maalum na Serikali?

Shahidi: Hapana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho Ijumaa, ambapo shahidi huyo ataendelea kuhojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa utetezi

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Dk. Mwakyembe : Zanzibar waliongoza kutaka Serikali 2 za muungano

Spread the love  MWANASIASA mkongwe nchini, Dk. Harrison Mwakyembe, amesema mjadala wa...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia ataja mikakati ya kufikia trilioni 2 biashara Uturuki, Tz

Spread the loveWakati Tanzania na Uturuki zikidhamiria kuongeza kiwango cha biashara hadi...

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

error: Content is protected !!