January 17, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi: Mbowe hakukamatwa sababu ya katiba

Spread the love

 

MRAKIBU wa Polisi, Jumanne Malangahe, amedai Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, hakukamatwa na Jeshi la Polisi Tanzania kwa sababu ya harakati za katiba mpya, bali alikamatwa kwa ugaidi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Malangahe ametoa madai hayo leo Jumanne, tarehe 11 Januari 2022, alipokuwa anahojiwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga.

Mbowe alikamatwa na Jeshi la Polisi, usiku wa kuamkia tarehe 21 Julai 2021, jijini Mwanza, akijiandaa kushiriki kongamano la kudai katiba mpya, lililoandaliwa na Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), na kuunganishwa na wenzake watatu, katika kesi ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya ugaidi.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi, yenye mashtaka ya ugaidi ni, waliokuwa makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Adam Kasekwa, Halfan Bwire Hassan na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Mahojiano kati ya Wakili Kidando na Malangahe, anayedaiwa kumhoji Mbowe baada ya kuletwa Dar es Salaam akitokea Mwanza, yalikuwa kama ifuatavyo;

Kidando: Uliulizwa pia kama unajua mshtakiwa Freeman Mbowe alikamatwa Mwanza, akiwa kwenye mkutano wa Katiba ukasema hufahamu, je nini unachofahamu?

Shahidi: Mbowe alikakamatwa kwa ugaidi na si suala la katiba na ndiyo maana hata katika kuandika maelezo yake, tulimhoji kwa tuhuma za ugaidi.

Wakili Kidando alimhoji Malangahe swali hilo, baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala, kumuuliza kama anafahamu Mbowe alikamatwa Mwanza akishiriki kongamano la katiba.

Mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo;

Kibatala: Unakubaliana na mimi Mbowe alikamatwa Mwanza akishiriki kongamano la katiba?

Shahidi: Sikuwepo Mwanza

Kibatala: Unafahamu moja wapo ya mbinu za viongozi madikteta katika nchi za kidikteta ni kuwapa wapinzani kesi za ugaidi na mifano iko mingi, unalifahamu hilo?

Shahidi: Hilo silifahamu

Kibatala: Kwa ufahamu wako wewe Polisi msomi, nchi kama Sweden inaweza kumkumbatia mtuhumwia wa ugaidi?

Shahidi: Siwezi kuiongelea Sweden, siijui na siwezi kujua condition zao zikoje

Kibatala: Unafahamu nchi zote nilizotaja zinatuma wawakilishi kufuatilia kesi ya Mbowe?

Shahidi: Sijui, sijafahamishwa kuhusu hilo

Kibatala: Unafahamu maana ya travel advisory inayotolewa na balozi mbalimbali kunapotokea matishio ya kiusalama?

Shahidi: Binafsi sijawahi kukutana na kitu kama hicho

Kibatala: Uliwahi sikia tahadhari yoyote iliyotolewa na nchi dunini kwa raia wao wawe na makini na mikusuanyiko isiyo ya lazima Tanzania kati ya Agosti 2020 na Julai 2021, uliwahi kusikia?

Shahidi: Sikusikia

error: Content is protected !!