October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi: Kwa sasa ni kawaida polisi kuua

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu

Spread the love

MUSA Bakari, shahidi wa tano kwenye kesi inayomkabili Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo ameiambia mahakama kwamba ni kawaida polisi kuua. Anaripoti Faki Sosi, Dar es Salaam … (endelea).

Amedai, kwa sasa ni kawaida kwa Jeshi la Polisi kuua ingawa wajibu wake kisheria si kuua.

Musa ametoa kauli hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Kisutu, Huruma Shaidi leo tarehe 20 Machi 2020.

Amesema, amejitilea kutoa ushahidi kwenye kesi hiyo, baada ya kusikia Zitto anashitakiwa kwa uchochezi ilhali hakufanya uchochezi.

Shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa, ndio mara ya kwanza kumuona Zitto ana kwa ana na kwamba, alichokuwa akizungumza kwenye hotuba yake kimempendeza kwa kuwa aliitaka serikali ifanyie uchunguzi mauaji ya Mpeta, Kigoma.

Musa akiongozwa na wakili wa utetezi Bonifacia Mapunda, ameileza mahakama kuwa, siku ya tarehe 28 Oktoba 2018, akiwa kwenye eneo lake la biashara ya chips Tandika jijini Dar es Salaam, saa nne asubuhi akiperuzi kwenye mtandao wa YouTube, alikutana na mkutano wa waandishi wa habari na Zitto Kabwe ulikuwa ukirushwa Live (Mubashara).

Musa amedai, kwenye video hiyo Zitto alimpongeza mcheza mpira wa kimataifa Mbwana Samatta kwa namna anavyoiwakilisha nchi kimataifa.

Ameeleza, Zitto alizungumzia masula ya usalama wa nchi, kwamba watu wanatekwa, maiti zinazopatikana kwenye viruba kwenye fukwe za bahari na kutaka serikali iyafanyie uchunguzi matukio hayo.

Amedai kuwa, Zitto aliishauri serikali kufanyia uchunguzi tukio la kupotea kwa Azory Gwanda na kupigwa risasi kwa Tundu Lissu.

akihojiwa na wakili wa serikali mwandamizi Nassoro Katuga juu taswira yake kwa jeshi la polisi na serikali, baada ya kusikiliza hutuba ya Zitto.

Amedai kuwa, alimpongeza Zitto kwa kwa kuitakia mema nchi na kuishauri serikali juu ya usalama wa nchi.

Ameweka wazi hisia zake kuwa, hajalichukia jeshi la polisi kutokana na hutuba ya Zitto isipokuwa, alichukulia kawaida na litafanyia kazi ushauri wake.

Alipoulizwa juu ya kauli yake ya kuchukulia kawaida mauaji ya jeshi la polisi, ilhali kazi yao ni kulinda raia na mali zao?

Amejibu, anachukuliwa kawaida kwa kuwa suala hilo ni la kawaida.

Wakili Katuga: Polisi kuua raia kawaida?

Shahidi: kwa sasa ni kawaida.

Wakili Katuga: Wewe unaon kawaida polisi kua raia wameua kuanzi mwaka gani?

Shahidi: Sijui

Wakili Katuga: Jeshi la Polisi sio majukumu yake kuua raia, umesema kwa sasa ni kawaida kuanzi lini? mwaka jana?

Shahidi: Nimesema kawaida kwa sababu jeshi la polisi linafanyia kazi.

Wakali Katuga: Umesema jeshi la polisi kuua raia ni kawaida, unamaanisha nini?.

Shahidi: Nimemaanisha kawaida.

Wakili Katuga: Nini kilikusukuma kuja kutoa ushahidi?

Shahidi: Niliomba niwe shahidi baada ya kuona serikali inamwambia Zitto mchochezi ilhali sio mchechezi, ndio nikawasiliana na Wakili Bonifasia Mapunda ambaye niliwahi kukutana naye kwenye mahakama ya mwanzo ya Temeke.

“Niliona kwenye YouTube kuwa Zitto ana kesi ya kujibu kwenye kesi ya uchechezi, nami najua kuwa yeye hajafanya uchochezi,” amedai Mussa.

Shahidi amedai kuwa, alivutiwa na hutuba ya Zitto kwa kuwa, alikuwa akisema ambayo yametokea nyumbani kwako Rufiji ambapo anasema kweli kuwa kulikuwa na mauaji.

Awali, shahidi wa nne aliyejitambulisha kwa jina la Abubakari Kabumbula (40), mkazi wa Magomeni Mapipa ambaye alikuwa akisikiliza hotuba ya Zitto kupitia YouTube, aliyekuwa akizungumzia masuala ya korosho na usalama wa nchi.

shahidi huyo ameeleza kuwa, video hiyo alikuwa akitazama kwenye kijiwe cha Taxi mtaa wa Dosi, Magomeni na watu wengine ambao hawajui na kwamba aliuelewa ujumbe wa Zitto ulielekea kwa Jeshi la Polisi, juu ya kulitaka kufanyia uchunguzi matukio aliyoyaanisha kuwa yanahatarisha amani.

Hakimu Shaidi ameahirisha shauri hilo mpaka tarehe 2 na 3 Aprili 2020 kwa ajili ya kuendele na ushahidi wa upande wa utetezi.

error: Content is protected !!