Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Shahidi azungumzia madai ya Mbowe kukimbia upelelezi, kufikisha malalamiko kwa Rais
Habari za Siasa

Shahidi azungumzia madai ya Mbowe kukimbia upelelezi, kufikisha malalamiko kwa Rais

Spread the love

 

SHAHIDI wa 13 wa Jamhuri, katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, Tumaini Swila, amedai hakusikia taarifa zilizodai mwanasiasa huyo alitoroka nje ya nchi kukimbia upelelezi wa tuhuma zinazomkabili. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mkaguzi huyo wa Polisi ametoa madai hayo leo Jumanne, tarehe 15 Februari 2022, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joachim Tiganga wakati akiulizwa maswali ya ufafanuzi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo namba 16/2021, ambao walipandishwa kizimbani miezi 11 kabla ya mwanasiasa huyo, ni waliokuwa makomando wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Makomando hao wa JWTZ, walipandishwa katika kizimba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, tarehe 19 Agosti 2020 huku Mbowe akiunganishwa tarehe 26 Julai 2021.

Ambapo Inspekta Swila aliieleza mahakama hiyo kwamba Mbowe alichelewa kuunganishwa kwa kuwa upelelzi ulikuwa haujakamilika kwani walikuwa wanasubiri ripoti ya uchunguzi wa kisayansi ya simu za washtakiwa hao.

Mahojiano kati ya Wakili Kidando na Inspekta Swila yalikuwa kama ifuatavyo;

Kidando: Pia ulikuwa unaulizwa katika nafasi yako kama mpelelezi, kama ulifahamu kwamba kuna wakati wowote Mbowe aliwahi kutoroka nchini.

Wewe ukasema haikuwa jukumu lako kutoa taarifa kama Mbowe alitoroka nchini na ukasema haukuwahi kuona taarifa iliyopo kwenye jalada la kesi. Kwa nini ulisema haikuwu jukumu lako?

Shahidi: Nilikuwa nasema hivyo sababu taarifa za kufuatiliwa mwenendo kwa mshtakiwa namba nne Mbowe, nilijulishwa na Afande Kingai kwamba mtuhumiwa mmoja anafuatiliwa mwenendo wake bila kunijulisha ni nani anamfuatilia, lakini alinijulisha anafuatiliwa.

Na niliposema kwamba hakukuwa na taarifa zozote za mtuhumiwa namba nne kuhusu kutoroka, nilikuwa sijaithibitisha hiyo taarifa na wala sikusikia.

Wakati huo huo, Inspekta Swila alidai hakufuatilia taarifa zinazodai Mbowe alipeleka malalamiko yake kwa Rais na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, kwamba watu wake wamepigwa na yeye ametukanwa na vijana wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Wakili Kidando alimuuliza kama ifuatavyo;

Kidando: Pia katika kielelezo hicho hicho namba 13 kuna jambo uliulizwa hapa, ili niweze kukuuliza swali kwanza usome kipengele hiki, kuanzia neno kwamba mpaka neno hilo. Kuanzia hapa mpaka hapa.

Shahidi: Kwamba watu wake Mbowe wamepigwa na yeye mweyewe anatukanwa na vijana wa Sabaya, ameshawahi kufikisha malalamiko yake kwa mheshimiwa Rais, lakini hajasaidiwa kitu chochote.

Pia, amewahi mueleza IGP Sirro lakini alijibiwa kwamba atalifuatilia hili.

Kidando: Sasa wakili alipokutaka kurejea jambo hilo alikutaka u-comfirm kwamba Mbowe alifikisha malalamiko yake kwa Rais na IGP, vitendo hivyo ukasema hauku-comfirm kuhusiana na masuala hayo, kwa nini haukufuatilia?

Shahidi: Sikufuatilia kuthibitisha sababu mimi sikuwa nahusika, yaani hili tukio sikuhusika kulifuatilia na sijui kama aliliripoti kama jinsi walivyoeleza hawa

Wakili Kidando alimuuliza maswali hayo, Inspekta Swila, baada ya Kiongozi wa Jopo la Mawakili wa Utetezi, Peter Kibatala kumuuliza kama yeye alitoa taarifa ya kwamba Mbowe amekimbia nchini akikimbia upelelezi wake.

Wakili Kibatala alimuuliza Inspekta Swila kama ifuatavyo;

Kibatala: Unasema uliteuliwa kuwa mpelelezi na DCI not direct, kupitia Afande Kingai, wewe mpelelezi hukutoa taarifa kwa wakubwa zako kwamba ghafla Mbowe amekimbia nchini, amekimbia upelelezi wako?

Shahidi: Sijawahi, jukumu halikuwa la kwangu la kumfuatilia.

Kibatala: Katika faili uliona taarifa kuwa Mbowe ametoroka nchini kukwepa upelelezi, latika faili lako la upelelezi?

Shahidi: Sikuwahi kuona.

Shahidi huyo anaendelea kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!