Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Habari Shahidi augua, kesi ya Mbowe yaahirishwa
HabariTangulizi

Shahidi augua, kesi ya Mbowe yaahirishwa

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imeahirisha usikilizaji wa kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, kutokana na shahidi wa sita wa Jamhuri kutohudhuria mahakamani hapo, kwa sababu za kiafya. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kesi hiyo imeahirishwa leo Jumatano, tarehe 3 Novemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joackim Tiganga, baada ya upande wa jamhuri kupitia Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, kuomba ahirisho.

Wakili Kidando ameieleza mahakama hiyo kuwa, shahidi huyo ambaye alitarajiwa kuwa wa sita kati ya 24 ambao upande wa mashtaka umepanga kuwaita, amepata ugonjwa hivyo ameshindwa kufika mahakamani.

“Mheshimiwa Jaji tumempata shahidi tuliyepanga kuendelea naye leo lakini amepata tatizo la kiafya, amepata ugonjwa na kushindwa kuja mahakamani. Kwa sababu hiyo tunaomba ahirisho la kuleta shahidi mwingine kesho,” amesema Wakili Kidando.

Baada ya maombi hayo, Jaji Tiganga amewauliza upande wa utetezi ambapo kiongozi wa japo la mawakili, Peter Kibatala amesema hawana pingamizi.

“Kwa kufuata amri ya mahakama iliyokuwa imetolewa jana. Sisi kwa upande wetu tulikuwa tumejiandaa vizuri. Lakini kama wenzetu wanasema hivyo ndiyo ilivyo tunaomba wenzetu kesho wajitahidi, tuweze kuendelea ili tuweze kumalizia kwa wakati,” amesema Kibatala

Mara baada ya Kibatala kueleza hayo, Jaji Tiganga ameiahirisha kesi hiyo hadi kesho Alhamisi saa 3:00 asubuhi na watuhumiwa wataendelea kuwa mahabusu.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni, Halfan Hassan Bwire, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya ambao walikuwa makomandoo wa Jeshi la Ulinzi na Wananchi Tanzania (JWTZ).

Shahidi wa tano wa jamhuri katika kesi hiyo, alikuwa ni Mwanasheria wa Kampuni ya Mawasiliano ya MIC Tanzania Ltd (Kampuni ya Tigo), Fredy Kapala, ambaye alitoa ushahidi wake ulioonesha namna mtu anayedaiwa kuwa Freeman Mbowe alivyomtumia Sh.500,000, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Luteni Denis Urio.

Katika ushahidi wake, Kapala alieleza taarifa za miamala ya fedha ya namba inayodaiwa kuwa ya Mbowe 0719933386, ikiwemo muamala wa kituma kiasi hicho cha fedha kwenda kwenye namba inayodaiwa kuwa ya Luteni Urio 0787555200.

Katika kesi hiyo, Mbowe anadaiwa kutoa fedha zaidi ya Sh. 600,000 kwa ajili ya kufadhili vitendo vya ugaidi, pia anadaiwa alimuomba Luteni Urio amtafutie Askari Polisi waliostaafu au kufukuzwa kazi hasa makomandoo wa JWTZ, ili wamsaidie kutekeleza vitendo hivyo.

Shahidi wa nne alikuwa Anita Varelian Mtali, ambaye ni mfanyabiashara wa pombe aina ya mbege, aliyetoa ushahidi wake namna alivyoshuhudia washtakiwa wawili katika kesi hiyo, Kasekwa na Ling’wenya walivyokamatwa tarehe 25 Agosti 2020, maeneo ya Rau Madukani, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Anita alidai wakati watuhumiwa hao walipopekuliwa baada ya kukamatwa, walikutwa na dawa za kulevya, huku akidai Kasekwa alikutwa na silaha aina ya bastola.

Katika kesi hiyo, Kasekwa anatuhumiwa kumiliki silaha hiyo kinyume cha sheria pamoja na risasi tatu, ambavyo vinadaiwa vilipangwa kutumika katika vitendo vya ugaidi.

Shahidi wa tatu wa Jamhuri, alikuwa ni Coplo Hafidhi Abdllah Mohammed, aliyeeleza namna alivyofanya uchunguzi wa silaha, risasi na maganda, vinavyodaiwa kuwa alikamatwa navyo mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Kasekwa, ambapo alidai uchunguzi wake ulibaini vinafanya kazi.

Shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi hiyo ni Justine Elia Kaaya, aliyekuwa msaidizi wa Mkuu wa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Katika ushahidi wake, Kaaya alidai Mbowe alimtafuta mara tatu kati ya Novemba 2018 hadi Julai 2020, akimtaka ampe taarifa za watu wa karibu na Sabaya pamoja na mahali anapopenda kutembelea ili atume watu wa kumdhuru.

Shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi hiyo alikuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Kinondoni, ACP Ramadhan Kingai, aliyeieleza mahakama hiyo namna Jeshi hilo lilivyopata taarifa juu ya mipango ya Mbowe na wenzake ya kula njama za kufanya vitendo vya ugaidi, ikiwemo kulipua vituo vya mafuta, maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi na kudhuru viongozi wa Serikali, akiwemo Sabaya.

ACP Kingai alidai, Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), aliyemtaja kwa jina la Luteni Denis Urio, alimpa taarifa aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini, Robert Boaz, kwamba Mbowe anatafuta askari waliostaafu au kufukuzwa kazi, hasa makomandoo wa JWTZ, ili wamsaidie katika mipango hiyo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!