October 18, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi akwamisha kesi ya Mbowe

Freeman Mbowe akiwa mahakamani

Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, imeahirisha kusikiliza kesi ndogo ya kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, hadi Ijumaa, tarehe 24 Septemba 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kesi hiyo iliyopangwa kusikilizwa mfululizo, imeahirishwa leo Jumatatu, tarehe 20 Septemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Mustapha Siyani, baada ya upande wa jamhuri kuomba ahirisho ukidai shahidi wake alitakiwa kuendelea na ushahidi keso Jumanne, amepata changamoto za kiafya.

Kauli hiyo ilitolewa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Robert Kidando, baada ya shahidi wa tatu wa jamhuri, Konstebo Ricado Msemwa, kumaliza kutoa ushahidi wake mahakamani hapo.

Wakili Kidando alidai kuwa, shahidi huyo alipata ajali siku ya Jumamosi, na kuiomba mahakama hiyo itoe muda ili shahidi huyo apone.

Wakili huyo wa jamhuri alidai, tayari shahidi mwingine alishafika Dar es Dalaam, lakini kutokana na mipango yao shahidi aliyepata matatizo ya kiafya alitakiwa kuanza kwanza.

Baada ya maombi hayo yaliyoafikiwa na upande wa utetezi, Jaji Siyani  aliahirisha kesi hiyo hadi Ijumaa.

Kesi hiyo ndogo  lilitokana na mapinganizi ya Mawakili wa utetezi, wakiongozwa na Wakili Peter Kibatala, wakipinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi ya msingi, Adam Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama kielelezo na Kamanda Kingai, katika kesi ya msingi,  wakidai yalichukuliwa nje ya muda kisheria.

Pia, katika mapingamizi hayo walihoji kwa nini mtuhumiwa alihojiwa Dar es Salaam, badala ya Moshi mkoani Kilimanjaro alikokamatwa.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine ni,  Kasekwa, Halfan Bwire Hassan na Mohammed Ling’wenya.

error: Content is protected !!