November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi aeleza mikakati ya Mbowe kumdhuru Sabaya

Spread the love

 

JUSTIN Elia Kaaya, shahidi wa pili wa Jamhuri ameieleza Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Dar es Salaam, namna Mwemyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alivyomtafuta mara tatu ili amsaidie katika mipango yake ya kumdhuru Lengai Ole Sabaya, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Kaaya ametoa madai hayo leo Jumatano, tarehe 27 Oktoba 2021, akitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano mkoani Dar es Salaam, kwenye kesi inamkabili Mbowe na wenzake.

Kaaya aliwahi kuwa mfanyakazi wa Sabaya kuanzia 2017 alipokuwa Diwani mkoani Arusha, hadi Oktoba 2018, alipokuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, Kaaya amedai mara ya kwanza Mbowe alimtafuta Novemba 2018 akimtaka aonane naye, ambapo walionana wilayani Longido mkoa wa Arusha.

Kaaya amedai, baada ya kuonana naye, Mbowe alimtaka ampe taarifa kuhusu shughuli anazofanya Sabaya na watu anaofanya naye kazi wilayani Hai, Kilimanjaro, ambapo alimkatalia akimwambia kwa wakati huo hakuwa kwa Sabaya.

Kaaya amedai, Mbowe alimtafuta kwa mara ya pili Januari 2020 kupitia namba yake ya Airtel ya 0784779944, ambapo alimuomba akutane naye Moshi mkoani Kilimanjaro. Na kuwa alikutana naye Aishi Hotel iliyoko Machame mkoani humo, akiwa na mlinzi wake aliyemtaja Halfan Hassan Bwire.

Amedai, baada ya kukutana naye, Mbowe alimuomba amtajie majina ya wasaidizi wa Sabaya na namba zao za simu, kitendo alichokifanya. Baada ya hapo aliachana na mwanasiasa huyo.

Kaaya amedai, Mbowe alimtafuta kwa mara ya tatu Julai 2020, ambapo alionana naye mkoani Kilimanjaro, akiwa na dereva na mlinzi wake, Bwire, kisha alimuomba amtaje tena majina ya wasaidizi wa Sabaya na namba zao za simu, kitendo alichokifanya kwa kuyaandika katika karatasi kisha akampatia mlinzi wake.

Amedai, Mbowe alimtaka amtajie maeneo ambayo Sabaya anapenda kutembelea, akamtajia ikiwemo Klabu ya The Don, Mile Store Pack na Hoteli ya Gold Crest na SG Resort zilizoko jijini Arusha.

Shahidi huyo wa Jamhuri amedai, mlinzi wa mbowe, Bwire alisema Sabaya ni mtu mdogo sana hivyo atamchezesha.

Kaaya amedai, baada ya kumaliza kazi hiyo, Mbowe kupitia namba ya Airtel 0784779944, alimtumia Sh.200,000 kwenye namba yake ya Voda 0754916666 kisha akarudi nyumbani kwake Arusha.

Shahidi huyo amedai, baada ya kupewa fedha hizo, Mbowe alimwambia kazi imeanza rasmi na kwamba ataanza kumlipa mshahara.

Kaaya amedai, baada ya hapo tarehe 25 Julai 2020 alikamatwa na Jeshi la Polisi, akielekea benki ya CRDB jijini Arusha kuweka fedha za mauzo ya mazao yake na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Arusha.

Baadaye alisafirishwa kwenda Dar es Salaam na kuhojiwa na Askari aliyemtaja kwa jina la Afande Mahita.

Amedai, baada ya kuhojiwa alipelekwa mahabusu hadi siku aliyofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, na wenzake watatu alikofunguliwa mashtaka ya kushiriki vikao vya kupanga kutenda mambo ya kigaidi, kula njama za ugaidi na kesi ya utakatishaji fedha.

Kaaya amewataja wenzake kuwa ni, Bwire, Mohammed Abdillah Ling’wenya na Adam Kasekwa. Ambao waliwekwa wote katika mahabusu ya Gereza la Ukonga.

Amedai tarehe 26 Julai 2021 Mbowe aliletwa gerezani hapo, ambapo aliwaambia amekwenda kuwatoa.

Wakili Chavula alimuuliza alikuwa kwenye kesi hiyo kwa muda gani, amejibu akidai miezi 11.

Fuatilia haya mahojiano ya Wakili Chavula na Kaaya

Wakili wa Serikali: Baada ya kuwa umeunganishwa kwenye kesi hiyo Mahakama ya Kisutu ulipelekwa wapi?

Shahidi: Nilipelekwa Gereza la Ukonga.

Wakili wa Serikali: Ulikuwa na akina nani?

Shahidi: Kila amtu alikuwa na wing yake. Nilikuwa na Khalfani Bwire na baadae kaongezeaka mtu anaitwa Khalid Athuman na baadaye akaongezeka Mohamed Ling’wenya akitokea Segerea.

Wakili wa Serikali: Umekuwa kwenye kesi ile kwa muda gani?

Shahidi: Kwa miezi 11.

Wakili wa Serikali: Nini kilitokea?

Shahidi: Aliletwa Mheshimiwa Mbowe siku ya tarehe 26 Julai 2021. Alitukuta tukiwa na Khalfani Bwire, akasema poleni sana. Nimekuja kuwatoa.

Wakili wa Serikali: Baada ya kauli hiyo nini kilitokea?

Shahidi: Asubuhi watu wa Magereza walikuja kusema tujiandae tunaenda Mahakamani.

Shahidi: Kesho yake tarehe 27 Julai 2021 tulipelekwa Kisutu mbele ya Hakimu Mzee Simba mimi, Khalid Athuman (mshtakiwa wa tano) na Gabriel Muhina (mshtakiwa wa sita).

Mwanasheria akasema bada ya upelelezi kuwa sisi hatuhusiki kwa hiyo tumefutiwa mashitaka kwa kifungu kidogo. Baada ya pale niliondoka kutoka mahakamani kwenda kwa mdogo wake Kitunda. Kesho yake nikarudi mahakamani kwa Mwendesha Mashitaka kuuliza vitu vyangu.

Jaji: Ni sehemu ya ushahidi wenu kwamba alienda kwa mdogo?

Wakili wa Serikali: Hapana Mheshimiwa.

Shahidi: Kesho yake nilipokwenda Kisutu kuuliza utaratibu wa fedha zangu wakanielekeza niende Central Police Dar es Salaam. Nikaenda kuonana na Inspector Swila akaniandika maelezo. Baada ya kuniandika maelezo akanipa vitu vyangu.

Wakili wa Serikali: Umemtaja mtu anaitwa Freeman Mbowe, Khalfani Bwire, Mohamed Ling’wenya …unaweza kuwatambua?

Shahidi: Ndiyo. Wapo hapa mahakamani.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji naomba sasa awatambue hapa mahakamani.

Jaji: Upande wa utetezi?

Kibatala: Hatuna pingamizi.

Shahidi anakwenda walipo washitakiwa na kumtaja kila mmoja kwa jina lake.

Wakili wa Serikali: Mheshimiwa Jaji siye ni hayo tu.

Jaji: Upande wa utetezi? Mkizingatia ni muda wa mapumziko.

Kibatala: Tunaweza za kushauriana nao?

Jaji: Ni sawa.

Kibatala: Tuna pendekezo kwamba tukuombe tu- break kwa dakika 30.

Jaji: Saa nane na dakika 25 tutarudi tena kuendelea.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali kujua kinachoendelea.

error: Content is protected !!