October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Shahidi aeleza Diwani CCM alivyopokea rushwa, alivyonaswa

Elias Mtarawanje

Spread the love

SHAHIDI wa kwanza Yusufu Shaban Omar Matimbwa katika kesi inayomkabili Diwani wa Kijichi, Mbagala jijini Dar es Salaam Elias Mtarawanje (29), anayedaiwa kupokea rushwa, ameeleza namna Polisi walivyoweka mtego na kufanikiwa kumnasa kiongozi huyo wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Shahidi huyo ambaye ni mwekezaji wa Hotel ya Giraffe Temeke jijini Dar es Salaam, leo Alhamisi tarehe 30 Julai 2020 amedai ana ushahidi wa kutosha kuithibitisha mahakama kuwa Diwani huyo alipokea rushwa ya sh milioni moja za mtego kutoka kwake.

Diwani Mtarawanji alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke mwaka huu, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kupokea rushwa ya Sh. 1 milioni kutoka kwa Matimbwa.

Akitoa utetezi wake mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama Wilaya ya Temeke, Catherine Madili, Matimbwa, amedai diwani huyo alimuomba kiasi hicho cha fedha, ikiwa ni sehemu ya Sh.20 milioni ili amsaidie kufanikisha haraka malipo ya zaidi ya Sh.200 milioni, anazoidai Halmashauri ya Wilaya ya Temeke iliyonunua kiwanja chake kwa zaidi ya sh milioni 500.

Amedai Halmshauri ya Wilaya ya Temeke ililichukua eneo hilo na kulitumia kama kituo cha daladala cha Kijichi, jijini Dar es Salaam

Amedai eneo hilo linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa ekari tatu, alilinunua kwa mtu aliyemtaja kwa jina moja la Mzee Mkumba, lakini kabla ya kuanza kulifanyia kazi Manispaa ya Temeke ililichukua kwa matumizi yake kinyume cha sheria.

Shahidi huyo ameeleza kwamba baada ya kuona Manispaa imenyang’anya eneo lake isivyo halali, alifungua kesi mahakama ya ardhi kuzuia taratibu za ujenzi zisiendelee hadi atakapolipwa stahiki zake.

“Baadaye niliandikiwa barua ya wito kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Temeke ili kuiondoa kesi mahakamani na kujadiiana nje. Tulifikia makubaliano nilipwe Sh.566 milioni.”

Ameieleza mahakama kwamba, Halmashauri ya Wilaya ya Temeke, ilimlipa awamu ya kwanza Sh.350 milioni ambazo alilipwa tarehe 4 Novemba, 2019 huku awamu ya pili ya Sh.216.35 milioni bado hajalipwa.

Almendelea kueleza wakati akiendelea kusubiri awamu ya pili ya malipo, Diwani Mtalawanje alikuwa akimpigia simu mara nyingi kutaka ampatie Sh.20 milioni ili amsaidie kulipwa madai yake mapema iwezekavyo.

Amedai kuwa kutokana na usumbufu wa kudaiwa kiasi hicho cha fedha, aliamua kwenda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kumlalamikia Diwani Mtawalawanje.

Baada ya kuwasilisha malalamiko yake hayo, maofisa wa Takukuru walimweleza kwamba arejee siku inayofuata kwa ajili ya kufanikisha malalamiko yake.

Akaieleza mahakama hiyo kwamba, siku inayofuata, diwani huyo alimsumbua mara kadhaa kwa lengo la kuhitaji fedha hizo, hali ambayo ilisababisha shahidi huyo alipeleke jambo hilo, Polisi Temeke kwa lengo la kujiweka katika utulivu.

Polisi Temeke walimshauri kwamba amtegee mtego, diwani huyo ili wakamkamate na rushwa ambako walimpatia fedha za moto ambazo aliondoka nazo hadi ofisini kwake.

Alipotoka Polisi Temeke, diwani Mtalawanje alimpigia simu mwekezaji huyo akimsisitiza kuhusu kiasi alichokitaka, akamwambia akubali kupokea shilingi milioni moja.

Amedai kuwa walikubali wakutane siku ya pili ofisini kwake na alifika na mtu mwingine ambaye alimtambulisha kuwa Katibu wa CCM kata ya Mgeninani.

Amedai kuwa lipofika ofisini kwake alimkabidhi fedha hizo ambazo Diwani huyo aliziweka kwenye bahasha na kumkabidhi Katibu wa CCM ambaye alikuja naye.

Alipopokea fedha hizo, wawili hao walikamatwa na polisi ambao walikuwa wameweka mtego huo.

Shauri hilo litaitwa kwa mara nyingine, tarehe 10 Agosti,2020 kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

error: Content is protected !!