May 5, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sh.6 trilioni zalipa deni la Serikali, wastaafu 57,605 kicheko

Dk. Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania imesema, kati ya Julai 2019 na Machi, 2020 imelipa mafao na pensheni kwa wastaafu wa Serikali 57,605, mirathi kwa warithi 1,006 na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi 457 wa Serikali walio kwenye mikataba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma

Hayo yamesemwa leo Ijumaa bungeni tarehe 15 Mei, 2020 na Dk. Philip Mpango wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi kwa wizara yake ya mwaka 2020/21.

Amesema wizara inawajibika kulipa mafao na pensheni kwa watumishi wa umma ambao hawachangii katika mifuko ya hifadhi ya jamii, mirathi na malipo ya kiinua mgongo kwa watumishi wa Serikali walio katika mikataba na viongozi wa kisiasa.

Dk. Mpango amesema,  wizara imeendelea kufanya uhakiki wa Daftari la Pensheni kila mwezi kabla ya malipo; kuandaa vitambulisho vipya vya wastaafu vya kielektroniki katika mfumo wa “smart cards” na kuboresha Mfumo wa unaotumika kutoa huduma kwa njia ya mtandao na kudhibiti fedha za mirathi zinazotoka Hazina kwenda moja kwa moja kwenye akaunti za warithi (Tanzania Pensioners Payment System – TPPS).

Akizungumzia deni la Serikali, Dk. Mpango amesema wizara inaendelea kusimamia Deni la Serikali kwa kuzingatia Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura 134.

Amesema kipaumbele ni kukopa kutoka kwenye vyanzo vyenye masharti nafuu na fedha zinazopatikana kuelekezwa kwenye miradi ya maendeleo, hususan miradi inayochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi na maendeleo ya watu.

Waziri huyo amesema, wizara inaendelea kuhakikisha kuwa, madeni yote yanayoiva yanalipwa kwa wakati.

“Hadi kufikia mwezi Machi 2020, Serikali ilifanikiwa kulipa deni lake lote lililoiva lenye thamani ya Sh.6.19 trilioni. Kati ya kiasi hicho, deni la ndani ni Sh.4.06 trilioni ikijumuisha riba Sh1.08 trilioni  na mtaji Sh.2.98 trilioni,” amesema Dk. Mpango

“Aidha, deni la nje ni Sh.2.13 trilioni ikijumuisha riba ya Sh.636.75 bilioni na mtaji Sh1.49 trilioni,” amesema

Dk. Mpango amesema kwa mwaka 2020/21, wizara itaandaa na kutekeleza mikakati itakayowezesha Serikali kukopa katika soko la fedha la ndani na nje bila kuathiri uhimilivu wa deni la Serikali, Sheria ya Mikopo, Dhamana na Misaada Sura 134 na vigezo vya viashiria hatarishi vya madeni yaliyotokana na dhamana za Serikali.

error: Content is protected !!