July 24, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Sh. 300,000 zavuruga mkutano Dar

Spread the love

VUTA nikuvute kati ya wakazi wa Serikali ya Mtaa wa Kibangu iliyoko Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na uongozi wa mtaa huo imesababisha mkutano kuvunjika baada ya Mwenyekiti Desdery Ishengoma kugomea wito wa kuwasilisha taarifa ya mapato na matumizi, anaanidka Timothy Kahoho.

Mkutano huo ulifanyikia Shule ya Msingi ya Kibangu tarehe 28 Februari, 2016 ambapo Ishengoma alikuwa akitakiwa na wajumbe wake kutoa taarifa ya mradi wa mabasi yaendayo Makoka yakitokea Kituo cha Kibangu kwa kutozwa Sh. 500 kila moja.

Kuvunjika kwa mkutano huo kulizua tafrani kwa baadhi ya wajumbe kumtuhumu mwenyekiti wao kuwatumia vijana saba katika kukusanya Sh.55,000 kila siku kutokana na mabasi yanayosafirisha abiria kutoka Kibangu kwenda Makoka.

Mkutano wenyewe ulianza saa 5.30 asubuhi kwa kufunguliwa na mwenyekiti ili kujadili dondoo zinazohusu namna ya kutunza usafi wa mazingira ya mtaa huo, suala la Kituo cha Mabasi yaendayo Makoka, ukosefu wa maji safi na kutofanyika vikao vya serikali ya mtaa huo.

Akianza na utunzaji wa usafi wa mazingia yao, alielezea kukithiri kwa uchafu kutokana na kukosekana mkandarasi wa kuzoa taka baada ya walioteuliwa kutimka kwa madai ya kutolipwa ada zao kutoka kwa wakazi wa mtaa huo. Alidai kuwa yote hayo ni kutokuwepo kamati ya afya ili kufuatilia hali ya usafi kwa ujumla.

Ufafanuzi wake huo ulisababisha asakamwe na baadhi ya wajumbe kuwa ni miaka 7 tangu achaguliwe kushika madaraka haweza kuitisha kikao chochote na hivyo yeye kuwa chanzo kikuu cha mlundikano wa uchafu katika mtaa mzima.

“Tatizo la taka ni wewe kupuuzia agizo la Rais Magufuli kuhusu utunzaji wa mazingira ya mtaa wetu,” alilalamika Katani Manyele.

Manyele alisema huwa wanalipa kodi za majengo na biashara lakini haoni ni kwa nini wakose huduma ya mkandarasi wa kuzoa taka kwenye mtaa wao.

Mjumbe mwingine alisikika akidai kutokuwa na imani naye kwa sababu hana uhalali wa kuongoza serikali ya mtaa wao baada ya kushindwa kusoma muhtasari wa mkutano uliopita na pia kutowasilisha mapato na matumizi katika vipindi vyake vya uongozi wake tangu mwaka 2009.

“Umetueleza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni imekuwa ikitoa Sh.30,000 kila mwezi kwa ajili ya kuendeshea ofisi, mbona hujatusomewa taarifa ya mapato na matumizi ya ruzuku hiyo?” alihoji mjumbe huyo.

Hata hivyo, Ishengoma alijitetea kuwa ofisi yake haikuwa na Katibu Mtendaji kwa muda mrefu kwa kuwa ndiye anayehifadhi nyaraka zote za ofisi, hiyo ikachochea kumkomalia kwa kusema ubavuni mwake yupo Katibu Mtendaji, Dandas Kijo.

Aidha, mwenyekiti huyo alisema Mtaa wa Kibangu unawahusu watu wote na kama wana nia ya kumuondoa ni lazima wafuate utaratibu, lakini siyo kwenye mkutano huo ulioitishwa na uongozi.

Ni baada ya kudai hivyo, aliletwa mjukuu wake akidaiwa kubugia vidonge vingi na kusababisha Ishengoma atelekeze ghafla mkutano huo na kasha akamchukua mjukuu wake huyo kwa kigezo cha kumkimbiza hospitalini na kuacha mvutano.

Kiongozi huyo inasemekana alishika kiti hicho kwa mara ya kwanza mwaka 2007 kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Aligombea tena na kushinda nafasi hiyo katika uchaguzi wa serikali za mitaa vitongoji na vijiji wa 14 Desemba 2014 hadi siku hiyo ulipofanyika mkutano wa wakazi wote na kuvunjika huku akidaiwa kusunda Sh.300,000 kila mwezi kutokana na mradi wa kukusanya ada kwa mabasi yaendayo Makoka.

error: Content is protected !!