JAMES Rugemalira (74), bado anasota kwenye gereza la Segerea, jijini Dar es Saalaam. Anashitakiwa kwa kuhujumu uchumi. Anaripoti Saed Kubenea … (endelea).
Anadaiwa kujipatia kinyume cha taratibu, mabilioni ya shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow, kupitia kampuni yake ya VIP Engineering and Marketing Limited.
Rugemalira alikuwa akimiliki asilimia 30 ya hisa katika kampuni ya kigeni ya IPTL kupitia kampuni yake hiyo.
Alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, tarehe 19 Juni 2017 na kusomewa mashtaka sita, yakiwamo ya uhujumu uchumi.
Mshitakiwa mwingine katika kesi hiyo, ni Harbinder Sigh Seth (Singasinga). Seth anadai kumiliki kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL), kupitia kampuni yake ya Pan African Power Tanzania Limited (PAP).
Mabilioni ya shilingi yaliyokuwa yamehifadhiwa katika akaunti ya Escrow yalikwapuliwa na Singasinga huyo aliyejiita mmiliki wa IPTL kwa msaada mkubwa wa viongozi wakuu wa serikali na kile kilichoitwa, “amri ya mahakama.”
Hata hivyo, kinachoitwa amri ya mahakama, kilikuwa ni kumaliza mzozo wa wanahisa wa IPTL na mbia mwenzake kampuni ya Rugemalira na kampuni ya MECHMAR ya Malaysia.
MECHMAR ilikuwa inasisitiza na mpaka sasa, bado inasisitiza, kuwa mtambo wa IPTL uliyopo eneo la Tegeta, Salasala, jijini Dar es Salaam, ni mali ya Benki ya Standard Chartered ya Malaysia.
Benki ya Standard Chartered ilikuwa inadai na mpaka sasa bado inadai kuwa mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na fedha zilizopo kwenye akaunti ya Escrow, ni mali yake.
Inadai kuwa kampuni ya MECHMAR ya Malasia ilishindwa kurejesha mkopo iliochukua benki na kwamba hilo ni jambo linalosababisha mitambo ya IPTL iliyopo Tegeta Salasala, jijini Dar es Salaam, kuwa mali yake.
Standard Chartered inaeleza kuwa ilikabidhiwa mamlaka ya kumiliki, kusimamia na kuendesha, mitambo ya kuzalisha umeme ya IPTL na mahakama, kufuatia MECHMAR kushindwa kulipa mkopo.
Mkataba huo ulipa benki ya SCB haki za IPTL ndani ya mkataba wa kuuziana umeme (PPA) na kumiliki mtambo wa kuzalisha umeme wa IPTL.
Benki ya Standard Chartered inaidai Tanesco dola za Marekani 258.7 milioni kama deni linalotokana na gharama za umeme uliozalishwa na IPTL na dola za Marekani 138 milioni zinazotokana na mkopo pamoja na riba.
Kwa mujibu wa uchambuzi wa vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na kimataifa, wanasheria waliobobea kwenye mikataba na mawakili wanaotetea Shirika la umeme la taifa (Tanesco), IPTL na serikali, madai hayo ni halali kwa mujibu wa sheria.
Akihutubia taifa kupitia walioitwa, “wazee wa mkoa wa Dar es Salaam,” wiki tatu baada ya Bunge kuagiza waliohusika katika wizi wa fedha za Escrow kuchukuliwa hatua, Rais Jakaya Mrisho Kikwete alisema, “…fedha za Escrow siyo mali ya umma.”
Kwa mujibu wa Kikwete, “Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wakati wa ukaguzi wa mahesabu ya Tanesco, ameeleza kuwa fedha za Escrow ni mali ya IPTL. CAG aliagiza fedha hizo ziondolewe kwenye hesabu za Tanesco kwa kuwa siyo mali yake.”
Hata hivyo, Rais Kikwete alikiri kuwapo udanganyifu katika kufikia utoaji wa fedha za Escrow.
Alikiri baadhi ya nyaraka kughushiwa. Akakiri kuwa kampuni ya PAP imekwepa kodi ya serikali na kudai kuwa serikali yake bado inaendelea kuitafuta kampuni ya MECHMAR iliyodaiwa kuuza asimia 70 ya hisa zake ndani ya IPTL.
Aidha, Rais Kikwete alikiri kuwa aliyepewa fedha na serikali – PAP – hakuwa na sifa; serikali yake haikufanya uchunguzi yakinifu kuhusu historia, uhalali, sifa na uwezo wa kampuni ya PAP katika uwekezaji wa umeme, ununuzi wa mitambo na mtaji.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya serikali, Sethi alitokea ikulu kabla ya kukwapua zaidi ya Sh. 321 bilioni kutoka akaunti ya Escrow katika Benki Kuu ya taifa (BoT).
Aidha, anayejiita na kuitwa na serikali kuwa ni “mmiliki mpya wa IPTL/PAP,” Harbinder Singh Sethi, aliletwa nchini na mmoja wa wanafamilia wa Rais Kikwete.
Mara baada ya kutoka ikulu jijini Dar es Salaam na kukutana na “wakubwa;” na kutoka hapo singasinga alikwenda moja kwa moja kukwapua mabilioni ya shilingi BoT hata bila kumfahamisha Rugemalira – mbia mwenzake.
Katika hili la IPTL, taarifa zinasema, Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Benno Ndullu alichukua tahadhari zote juu ya fedha hizo, ikiwamo kumjulisha aliyekuwa Waziri wa Fedha, umuhimu wa kumjulisha Rais Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu malipo hayo.
Gavana alikwenda mbali zaidi. Alitaka kupata uhakika kwamba utekelezaji wa uamuzi wa mahakama, pamoja na makubaliano ya kukabidhi fedha, unapata baraka za wakuu wa nchi kama vile Rais na Waziri Mkuu.
Pia BoT ilihakikisha kwamba mahitaji yote ya msingi kama vile, makubaliano ya kuhamisha fedha, kinga dhidi ya madai au mashitaka baada ya malipo, na suala la kodi ya ongezeko la thamani (VAT), vinapata ufafanuzi, baraka na mwongozo unaostahili.
BoT iliamua kuchukua hatua hizo ili kujinasua na madai mapya ambayo yangeweza kuibuka baada ya fedha kuhamishwa kutoka benki.
Kwa mujibu wa nyaraka, BoT ilihamishia mabilioni hayo ya shilingi kwa PAP kupitia akaunti yake iliyoko benki ya Stanbic baada ya Sethi, anayedai kuwa mmiliki wa IPTL, kumuelekeza gavana.
Waraka wa Sethi kwenda kwa gavana Ndulu ulielekeza fedha hizo kulipwa kwa akaunti Na. 9120000125324, iliyopo benki ya Stanbic, tawi la Tanzania.
Sethi alimwandikia gavana tarehe 28 Novemba 2013, zikiwa siku 37 (21 Oktoba hadi 28 Novemba 2013) tangu mkataba kati ya serikali na PAP kufungwa.
Mkataba wa upelekaji fedha katika akaunti ya Escrow ulifungwa tarehe 21 Oktoba 2013.
Malipo hayo kwa PAP yalifanyika bila Waziri wa Nishati, Prof. Sospeter Muhongo, wala BoT kuhakiki uhamishaji wa hisa kutoka Mechmar kwenda PAP; bila PAP kusajili hisa zake nchini; bila PAP kuthibitisha kujisajili Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC); na bila kuwa na hati ya mlipa kodi (TIN).
Mkataba kati ya serikali na IPTL ulielekeza fedha zilizohifadhiwa katika akaunti ya Escrow, zilipwe kwa kampuni ya PAP kupitia tawi la Tanzania la United Bank Limited (UBL) – yenye matawi zaidi ya 1,300 katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Qatar, Yemen, Marekani, Pakistani, Uingereza, Uswisi, Oman, China na Tanzania.
Mkataba huo uliagiza fedha hizo zilipwe kupitia akaunti mbili za PAP; ambazo ziko katika benki ya UBL. Akaunti hizo ni zile zenye Na. 010-0016-0 – ambayo ni ya fedha za Tanzania na 060-0016-7 ya dola za Marekani.
Katika moja ya maandishi yake, Rugemalira anahoji: “Tanesco inaweza kununua huduma ya umeme kutoka IPTL na badala ya kuilipa IPTL ikajilipa yenyewe?”
Alikuwa akimueleza rais Kikwete kile alichoita, “maswali yanayoombewa majibu kwenye sakata la TEGETA ESCROW.”
Rugemarila alifanya mawasiliano na Kikwete tarehe 29 Novemba 2015.
Akiandika kwa rais Kikwete, mmiliki huyo wa IPTL alisema, “kama kuna madai au makosa, kwenye mchakato wa kumaliza suala la IPTL, walalamikaji wamepewa ruhusu na Jaji John Utamwa, tarehe 5 Septemba 2014, kupeleka malalamiko yao mahakamani.
Akahoji, “ni busara Bunge liamrishe serikali kufuta hukumu ya mahakama?” Rugemalira alikuwa akieleza rais jinsi maamuzi ya Bunge yaliyoagiza serikali kutaifisha mtambo wa IPTL yasivyoweza kutekelezeka.
Alisema, “…serikali inayo mamlaka ya kutaifisha mali ya mtu binafsi bila kupitia njia za sheria? Je, Bunge halina wajibu wa kuheshimu na kuimarisha utawala wa sheria nchini?”
Akaongeza, “tangu lini likawa jukumu la Bunge kudai pesa kwa niaba ya kampuni binafsi wakati kampuni hiyo imefungua madai mahakama za nje kwa kisingizio cha kutokuwa na imani na mahakama zetu?”
Alisema, “tuelewe kwamba sasa Bunge letu linapiga kura ya kutokuwa na imani na mahakama iliyoanzishwa kwa mujibu wa Katiba?”
Rugemalira alihoji, “ni halali kwa watu wa nje pamoja na mashirika ya nje na wengine kutoka ndani, kutoa misaada, lakini ni haramu kwa kampuni yake ya VIP au yeye binafsi kufanya hivyo?”
Anasema, kama tozo ya uwekezaji wa IPTL ni wizi, serikali imejiridhisha kuwa tozo za makampuni mengine, ikiwamo Songas, Symbion na Aggreko kama siyo wizi mkubwa zaidi.
Anashauri kama kuchunguza IPTL, serikali inapaswa kuchunguza kwanza makampuni hayo ya kigeni.
Anasema, “kama fedha za IPTL ni haramu, kwa nini TRA wametoza kodi kwenye fedha ambazo zinadaiwa kuwa ni za wizi?”
Kampuni ya IPTL – Independent Power Tanzania Limited – ilijifunga katika mkataba na serikali wa miaka 20 wa kuzalisha megawati 100 za “umeme wa dharura” na kisha kuuza umeme huo kwa shirika la umeme la taifa (TANESCO).
Akaunti ya Tegeta Escrow ilifunguliwa mwaka 2004 baada ya serikali kushuku udanganyifu katika gharama za ununuzi wa umeme na mtaji wa IPTL.
Kampuni hiyo binafsi ilidai kuwa gharama za umeme zilikuwa asilimia 22.3; na gharama za mtaji asilimia 30 zilikuwa dola za Marekani 38.16 milioni. Hata hivyo, mahakama ilithibitisha kuwa gharama halisi za mtaji wa IPTL, zilikuwa chini ya dola za Marekani 1,000.
Hadi Novemba 2014, akaunti hiyo ilikuwa imehifadhi zaidi ya dola 120 milioni. Mamilioni hayo ya dola yaligawanywa mithili ya “shamba la bibi” kwa aliyejiita mwekezaji mpya wa IPTL, kampuni ya Pan African Power (PAP).
Mabilioni ya shilingi yalilimbikizwa na Tanesco, katika akaunti hiyo, baada ya kuibuka mgogoro juu ya malipo ya gharama ya uwekazaji wa mitambo na gharama za kuweka mitambo (Capacity Charge), kati ya IPTL na Tanesco.
Lakini fedha hizo zilichotwa kabla mgogoro huo haujapatiwa ufumbuzi na katika mazingira ya udanganyifu; na kwa kutumia baadhi ya nyaraka ambazo zilikuja kugundulika kuwa ni za kugushi.
Sethi aliwasilisha serikalini nyaraka zinazomuonesha kuwa ndiye mmiliki mpya wa IPTL. Hata hivyo, Sethi alishindwa kuweka uthibitisho wowote kuwa kampuni hiyo inamiliki hisa za kampuni ya Mechmar Limited ya Malaysia ndani ya IPTL.
Leave a comment