May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali Z’bar yakipongeza Chuo cha Mwalimu Nyerere, yatoa maagizo

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah

Spread the love

 

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdullah, amekipongeza Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha kinatoa wahitimu wenye uzalendo, weledi na uadilifu katika uongozi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hemed alitoa kauli hiyo jana Jumatatu tarehe 26 Julai 2021, wakati akiwe jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa chuo hicho kwa Kampasi ya Karume Zanzibar ambayo yameanza kujengwa kwa kutumia mapato ya ndani ya chuo hicho.

Alisema chuo kinatoa wahitimu waliobobea katika fani zao na wenye weledi katika masuala ya uongozi, maadili na utawala bora kitu ambacho kinaongeza tija katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Makamu huyo wa pili wa Rais aliwasisitiza wadau wa maendeleo kuchangia ujenzi wa mabweni hayo ya wanafunzi kwani kukamilika kwa ujenzi huo kutasaidia kutatua changamoto ya malazi kwa wanafunzi 1536 chuoni hapo.

“Nampongeza Mbunge wa Mpendae kwa niaba ya Turky Foundation amechangia Sh.20 milioni ikiwa ni jitihada katika kuchangia uboreshaji wa elimu hapa Zanzibar.”

“Natoa wito kwa wadau wa maendeleo waliopo Zanzibar kujitokeza kusaidia kufanikisha mradi huu utakao gharimu Sh.15.2 bilioni,” alisema Hemed

Pia, alimtaka mkandarasi wa mradi huo SUMA JKT kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa ufanisi.

Akizungumzia suala la uvamizi wa eneo la chuo na wauzaji wa dagaa, Hemed ameahidi suala hilo litamalizwa ndani ya kipindi kifupi kijacho hivyo chuo kiendelee kuwa na uvumilivu katika hilo.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho, Stephen Wasira alisema chuo kimeendeleza dhima ya kuanzishwa wake kwa kuwa kitovu cha kutoa elimu ya uongozi ,uzalendo, maadili na utawala bora.

Akizungumza na hadhira katika hafla hiyo, mkuu wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Prof. Shadrack Mwakalila ameishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kukisaidia chuo katika ukuaji wake na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikikabili Chuo hicho.

Makamu wa Pili wa Rais ameweka jiwe la msingi la mabweni chuoni hapo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

error: Content is protected !!