December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Prof. Lipumba awageuka washirika wake

Prof. Ibrahimu Lipumba, Mwenyekiti wa CUF

Spread the love

PROF. Ibrahim Lipumba, mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), ameungana na vyama vingine makini vya upinzani nchini, kukiondoa chama chake, katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam, leo tarehe 12 Novemba 2019, Prof. Lipumba amesema, hakuna sababu ya wanachama wa CUF kushiriki uchaguzi aliouita, “haramu mbele ya umma.”

Uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, umepangwa kufanyika nchini kote, Novemba mwaka huu.

Amesema, “CUF hatuutambui uchaguzi huu na viongozi wake watakaotangazwa. Hii ni kwa sababu, uchaguzi huu siyo halali. Viongozi  hawajachaguliwa na wananchi; bali wamechaguliwa kwa njia ya hujuma iliyofanywa na wasimamizi wa uchaguzi.”

Prof. Lipumba alisema, kauli yake hiyo, inatokana na maazimio ya Baraza Kuu la uongozi la taifa la CUF, lililokutana jana jijini Dar es Salaam.

Ametolea mfano wa kilichotokea wilayani Liwale, mkoani Lindi, ambapo amepataja kuwa ni ngome ya chama hicho. Amesema, katika jimbo hilo, “hakuna hata mgombea wa CUF aliyepita kwenye chujio la uteuzi.”

Amesema, vitendo vya kuhujumu upinzani vilianzia kwa wasimamizi wa uchaguzi kufunga ofisi na wale wachache waliotoa fomu, waligoma kuzipokea ziliporejeshwa.

Amesema, “zaidi ya asimilia 90 ya wagombea wetu wameondolewa kwenye uchaguzi huo, hivyo hatuna sababu ya kuendelea na uchaguzi huu.”

Taarifa kwamba CUF imejiondoa katika uchaguzi huo, zinakuja katika kipindi ambacho vyama vingine vitanne vya upinzani nchini Tanzania, vikitangaza kutoshiriki uchaguzi huo.

Vyama ambavyo vimetangaza kujiondoka katika uchaguzi huo, ni ACT- Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR- Mageuzi na Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA).

Akitangaza maamuzi ya chama chake, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, mjini Dodoma, tarehe 7 Novemba 2019, chama chake haitashiriki uchaguzi huo, kufuatia serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuamua kuwatumia watendaji wa mitaa, kuvuruga uchaguzi kwa maslahi ya chama hicho.

Alisema, “Kamati Kuu (CC) ya Chadema, imeamuru wanachama wake wote, viongozi na wafuasi kote nchini, kususia kwa kadri wanavyoweza, zoezi linaloendelea sasa la uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji.”

Kwa mujibu wa Mbowe, mbali na kususia uchaguzi, Chadema hakitawatambua viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi huo.

Naye Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo alisema, vikao vya juu ya chama chake, vimekubaliana kukiondoa chama chao kwenye uchaguzi huo.

Zitto amesema, “uchaguzi umevurugwa kwa kiwango ambacho hauwezi kurekebishika.” Akataka serikali kuufuta kuanzia wakati wa uchukuaji fomu.

Kwa upande wake, James Mbatia, mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, ameeleza kuwa kushiriki uchaguzi ambao kila mmoja amejiridhisha kwamba unaendeshwa kinyume cha sheria, ni kubariki haramu kwa kutaka kuifanya kuwa halali.

Mwenyekiti wa CHAUMMA, Hashimu Rugwe, yeye alifika mbali zaidi kwa kusema, chama chake “hakitashiriki uchaguzi huo, hadi hapo tume huru ya uchaguzi itakapoundwa.”

“Sisi tunataka Tume Huru ya uchaguzi, ambayo sisi sote tutaenda kuilalamikia. Haya mambo yanayofanyika sasa, yanatia uchungu na yasipochukuliwa hatua madhubuti kuyazuia, yanaweza kuingiza nchi kwenye machafuko,” ameeleza.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema, uamuzi wa chama hicho cha upinzani kujiondoa katika uchaguzi huo, unatajwa kuwa litakuwa pigo kubwa kwa CCM, kufuatia madai kuwa katika siku za karibuni CUF kimekuwa kikitumiwa na chama hicho tawala, kuvigawa vyama vya upinzani.

“Hakuna shaka kuwa sasa, CCM kitabaki pekee yake kwenye uchaguzi huu, baada ya washirika wake CUF, nao kuamua kujiondoa,” ameeleza mbunge mmoja wa upinzani ambaye hakupenda kutajwa gazetini.

Akizungumzia uchaguzi huo kwa undani, Prof. Lipumba amekwenda mbali zaidi kwa kusema, kiongozi yeyote atakayetokana na uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019, hawatomtambua.

Ameitaka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kutotumia nembo ya chama chake kwenye uchaguzi  huo.

“TAMISEMI isitumie nembo za CUF katika karatasi za uchaguzi. Sisi tumeshajiondoa. Hatuwezi kushiriki kwenye uchaguzi huu,” ameeleza Prof. Lipumba.

Amesema, pamoja na kuwa kuna mazingira ya kuminywa kwa demokrasia bado wanachama wa chama hiko wanajukumu la kukijenga chama chao.

error: Content is protected !!