Sunday , 29 January 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Serikali yazidi kuikomalia barua ya kina Mbowe
Habari za SiasaTangulizi

Serikali yazidi kuikomalia barua ya kina Mbowe

Spread the love

 

MAWAKILI wa Jamhuri katika kesi ya ugaidi, inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu, umemaliza kuwasilisha hoja zao za kupinga barua ya utetezi, kupokelewa kama kielelezo cha ushahidi. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Barua hiyo, iliandikwa na mawakili wa utetezi kwenda kwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar es Salaam ili kumuomba baadhi ya nyaraka kwa ajili ya kuzitumia katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya kupokelewa mahakamani.

Mawakili wa Jamhuri, waliweka pingamizi hilo jana Alhamisi, tarehe 25 Novemba 2021, mara baadaa ya Ling’wenya wakati akitoa ushahidi wake katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, kuiomba iipokee kama kielelezo.

Barua hiyo ilikuwa na lengo la kumuomba baadhi ya nyaraka ili kuthibitisha kama Askari Mpelelezi, Ricardo Msemwa, alikuwa msimamizi katika chumba cha mashtaka (CRO), cha Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam.

Kama alivyodai wakati anatoa ushahidi wake kwenye kesi hiyo ndogo, kuwa alimpokea Ling’wenya na mwenzake Adam Kasekwa, kwenye mahabusu ya kituo hiko, tarehe 7 Agosti 2020, ilihali washtakiwa hao wanakana hawakufikishwa na au kupokelewa na Msemwa, kituoni hapo.

Mawakili waandamizi wa Jamhuri, Abdallah Chavula na Pius Hilla walianza kutoa hoja zao za kupinga barua hiyo kupokelewa jana na wamehitimisha leo Ijumaa, tarehe 26 Novemba 2021 mbele ya Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo.

Wakili huyo Mwandamizi wa Serikali, Chavula leo ameendelea kufafanua hoja tatu zilizobakia, ikiwemo ya mnyororo wa uhifadhi wa barua hiyo (Chain of Custody), hadi kumfikia Ling’wenya, aliyeiomba mahakama hiyo iipokee kama kielelezo cha ushahidi wake, akidai haijajengewa misingi.

“Kwenye hoja ya chain of custody, ni mtizamo wetu mheshimiwa jaji kuwa katika eneo hili shahidi ameshindwa kuijenga na kuitengeneza. Hoja yetu sie katika eneo hili iko katika maeneo mawili, eneo la kwanza shahidi katika ushahidi wake ameeleza mahakama kuoneshwa barua hii.”

“La pili, shahidi ameionesha mahakama alimpa maelekezo wakili wake Fredrick aandike barua hii na barua hii inaonekana imeandikwa na Wakili Peter Kibatala, haijaelezwa imetoka vipi kwa Kibatala na kumfikia shahidi siku ya jana,” amedai Wakili Chavula.

Wakili Chavula amedai, ili barua hiyo ikidhi matakwa ya mnyororo wa utunzwaji kielelezo hadi kumfikia shahidi, inabidi kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Peter Kibatala, anayedaiwa kuandika barua hiyo, atoe ushahidi wake namna nyaraka hiyo ilivyomfikia kamanda huyo wa polisi na kurejeshwa mahakamani kwa ajili ya kuletwa kama kielelezo.

“Lakini kwa hali ilivyo, hata yeye mwenyewe hawezi kwenda pale kutoa ushahidi. Kwa hiyo, mnyororo wa uhifadhi wa nyaraka hii kuanzia ilivyopelekwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, mpaka kumfikia shahidi, jana mwenzetu Wakili Dickson Matata ameshindwa kumuongoza shahidi,” amedai Wakili Chavula.

Wakili Chavula amedai “pasipokuwa na ushahidi kama ilivyo hapa, mnyororo umekatika wa uhifadhi kielelezo na katika kukatika mnyororo wa hifadhi unaenda kuathiri uthibitisho wa hiki kielelezo.”

“Kwa hoja hizo, tunaiomba mahakama yako isipokee kielelezo hiki kwa sababu misingi ya uhifadhi wa kielelezo hiki kuanzia ilipotoka kwa mheshimiwa naibu msajili wa mahakama mpaka kumfikia shahidi hapa mahakamani siku ya jana,” amedai Wakili Chavula.

Wakili Chavula pia alitoa ufafanuzi kuhusu hoja yao ya barua hiyo kutokuwa na umuhimu kama ifuatavyo, “kwa kuwa ushahidi alioutoa awali unakinzana na kielelezo hiki, ni maoni yetu kwamba kielelezo hiki sio muhimu na kile ambacho shahidi amekizungumza.”

“Kwa mujibu wa kifungu cha saba cha sheria ya ushahidi sura ya sita kama ivyofanyiwa uhariri 2019, tulitegemea uletwe ushahidi wenye kuonesha uwepo wa hayo maelekezo aliyokuwa anayatoa mshtakiwa. Lakini kinacholetwa kinakinzana na alichokitoa ndiyo maana tunasema kielelezo hiki sio relevance,” amedai Wakili Chavula.

Wakili Chavula amefafanua hoja ya mwisho iliyodai shahidi huyo ameshindwa kujenga msingi wa kuikabidhi barua mahakamapo hapo, kama kielelezo cha ushahidi, akidai chanzo cha nyaraka hiyo sio yeye.

“Kushindwa kuthibitisha hivyo athari yake inaenda kuondoa uwezo wa kielelezo hicho. Kwa kigezo cha kushindwa kuweka msingi tunaomba mahakama hii isipokee barua hii sababu haina uwezo,” amedai Wakili Chavula.

Naye Wakili Hilla, amedai mshtakiwa huyo alishindwa kuthibitisha kilelezo hicho anachoomba kipokelewe mahakamani.

“Shahidi aliyepo kizimbani alishindwa kuthibitisha barua anayoomba ipoekelewe, uthibitisho ulitakiwa ufanyike, kabla ya kuomba nyaraka hiyo ipokelewe kwa mujibu wa ushahidi, uthibitisho ni suala la msingi.”

“Akitoa ushaidi wake alisema ataitambua barua kwa kutumia saini ya Kibatala hakusema ameipata lini wapi na kwa namna gani,” amedai Wakili Hilla na kuongeza:

“Hakuweza sema reference number ya barua hiyo, kuthibitisha unique future za barua hiyo. Kitu pekee alichosema anaweza kuitambua kwamba barua iko mikononi mwake. Ni wasilisho langu kwamba kwa mazingira yanayozunguka nyaraka hiyo jina lake pekee haitoshi kuithibitisha kwani yeye sio mwandishi wa barua hii,” amedai

Baada ya Wakili Chavula kumaliza kuwasilisha hoja hizo, mawakili wa utetezi wataanza kuzijibu.

Mbali na Mbowe, Ling’wenya na Kasekwa, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan Bwire ambao kwa pamoja wanatuhumiwa kupanga njama za vitendo vya ugaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi pamoja ja kudhuru viongozi wa serikali.

Endelea kufuatilia MwanaHALISI TV, MwanaHALISI Online na mitandao yetu ya kijamii kwa habari na taarifa mbalimbali

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

Haya hapa matokeo ya mtihani kidato cha nne 2022

Spread the loveBARAZA la Mitihani la Tanzania (Necta) leo Jumapili limetangaza matokeo...

Habari za Siasa

NCCR-mageuzi yawaangukia Polisi kupotea kwa kada wake

Spread the loveJESHI la Polisi nchini limeombwa kufanya uchunguzi wa kina utakaosaidia...

HabariTangulizi

Bakwata wamkangaa Sheikh wa Dar es Salaam

Spread the love  BARAZA la Ulamaa, limefutilia mbali uamuzi wa “kuvunja ndoa,”...

Habari za Siasa

Uamuzi kesi ya kupinga Bodi ya Wadhamini NCCR-Mageuzi kutolewa Februari 6

Spread the love  MAHAKAMA Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, imepanga...

error: Content is protected !!