Sunday , 3 December 2023
Home Habari Mchanganyiko Serikali yazidi kuikaba koo MwanaHALISI
Habari Mchanganyiko

Serikali yazidi kuikaba koo MwanaHALISI

Dk. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO
Spread the love

SERIKALI imeendelea ‘kulibana mbavu’ gazeti la kila wiki la habari za kiuchunguzi – MwanaHALISI kwa kuliagiza kuchapisha taarifa ya kumuomba radhi Rais John Magufuli katika ukurasa wa mbele wa toleo lake lijalo, anaandika Charles William.

Agizo hilo limetolewa leo na Dk. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari- MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, akisema mhariri na mchapishaji wa gazeti hilo wanapaswa kuchapa taarifa ya kumuomba radhi Rais Magufuli katika ukurasa wa mbele pasipo kukosa.

MwanaHALISI liliingia katika mvutano na serikali mapema Jumatatu ya wiki hii mara baada ya kuchapisha habari katika ukurasa wake wa mbele iliyokuwa na kichwa cha habari “Ufisadi ndani ya Ofisi ya JPM.”

Habari hiyo ilieleza mikataba mbalimbali ya kifisadi iliyoingiwa na Shirika la Elimu Kibaha lililo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambapo mikataba hiyo imeifanya Serikali kuambulia Sh. 320 milioni tu huku ikidaiwa deni la zaidi ya Sh. 9.7 bilioni.

Kilichoiudhi Serikali

Serikali kupitia kwa Dk. Abbasi msemaji mkuu, ilieleza kusikitishwa na habari hiyo kwa maelezo kuwa kichwa cha habari hiyo kililenga kumuhusisha moja kwa moja Rais Magufuli katika ufisadi huo hasa kutokana na kuwepo kwa maneno “Ofisini kwa JPM.”

Serikali ilitoa masaa 24 kwa gazeti hilo kumuomba radhi rais kutokana na taarifa hiyo, kwani imetengeneza taswira mbaya kwa kiongozi huyo ilihali ufisadi husika umefanywa na Shirika la Elimu Kibaha lililo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na si Ikulu.

Agizo hilo lilitekelezwa jana na MwanaHALISI kwa kutoa taarifa kwa umma pamoja na kuandika barua ya kuomba radhi kwenda serikalini.

Ndipo serikali imeibuka tena leo ikilitaka gazeti hilo kuchapa taarifa hiyo ya radhi katika ukurasa wake wa mbele kwenye toleo lijalo huku pia ikipongeza “mwitikio chanya” wa gazeti hilo dhidi ya amri ya serikali.

Utetezi wa MwanaHALISI juu ya kuihusisha Ofisi ya Rais

Gazeti la MwanaHALISI kupitia Mhariri wake Jabir Idrissa limefafanua kuwa kutokana na ufisadi husika kufanywa katika miradi ya maendeleo Shirika la Elimu Kibaha chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais Tamisemi, ndipo gazeti hilo lilichapisha kichwa husika cha habari katika toleo lake.

Idrissa amesema kuwa, gazeti hilo limekubaliana na ufafanuzi wa serikali kuwa Ofisi ya Rais Tamisemi haikupaswa kupewa uzito wa kuitwa “Ofisini kwa JPM” kwani ofisi halisi ya Rais ni Ikulu (State house) na ndipo likafikia hitimisho la kuomba radhi.

Itakumbukwa kuwa, Tamisemi ilikuwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu katika serikali ya awamu ya nne kabla ya Rais Magufuli kuamua kuihamishia katika Ofisi ya Rais kwa kile alichokieleza kuwa ni kutaka “kuongeza ufanisi.”

Licha ya kuhamishiwa katika ofisi ya Rais lakini utendaji wa Tamisemi unasimamiwa zaidi na Mawaziri husika ambao ni Waziri George Simbachawene na manaibu wake Angela Kairuki na Selemani Jafo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari MchanganyikoTangulizi

20 wafariki dunia kwa mafuriko Manyara

Spread the loveMVUA za vuli zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini zimeleta madhara...

ElimuHabari Mchanganyiko

CEO NMB awataka vijana kunoa ujuzi wao

Spread the loveAfisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, amewashauri...

Habari Mchanganyiko

TARURA kujenga madaraja 189 kwa teknolojia ya mawe

Spread the loveWakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imejipanga kujenga...

AfyaHabari Mchanganyiko

Majaliwa aipongeza GGML mapambano dhidi ya Ukimwi

Spread the loveWaziri Mkuu Kassim Majaliwa ameipongeza Kampuni ya Geita Gold Mining...

error: Content is protected !!