January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali “yawaziba midomo” viongozi wa dini

Waziri Mkuu Mstaafu na Mbunge wa jimbo la Munduli, Edward Lowassa akiwapokea wachungaji nyumbani kwake Dodoma

Spread the love

SERIKALI sasa imefungua makucha yake kwa viongozi wa dini. Hatua hii inatokana na matamko ya viongozi hao ya kuipinga Katiba inayopendekezwa pamoja na kuchangishana fedha za kumshaiwishi Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa agombee urais. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, serikali “imewafunga midomo” viongozi wa dini. Imesema wamekuwa wakitoa matamko yanayoashiria kungilia masuala ya kisiasa kinyume na sheria ya vyama, sura 337 na kanuni zake, pamoja na katiba zinazosimamia uendeshaji wa taasisi hizo.

Amri ya serikali inakuja wakati ambapo shinikizo la viongozi wa dini limeshika kasi hadi kuilazimisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha kura ya maoni iliyokuwa ifanyike 30 Aprili mwaka huu.

Viongozi wa dini na makundi mengine ya kijamii, wanasema kulazimisha kura hiyo kungechochea machafuko kwani uandikishaji wa wapigakura kwa mfumo wa BVR unaoendeshwa na NEC haujakamilika katika mkoa hata mmoja.

Mbali na hilo, maaskofu wanaounda Jukwaa la Kikristo, walikwenda mbali zaidi katika matamko yao wakiwataka waumini wao kuipigia kura ya hapana katiba inayopendekezwa kwa kile walichodai kuwa mchakato wake ulikuwa haramu.

Bila shaka matamko hayo ndiyo yameikwaza serikali, ingawa haikuwaja moja kwa moja maaskofu. Lakini waziri Chikawe amesema “Kwa mfano viongozi wa taasisi za dini wanapokutana na kutoa matamko yanayolenga kuwashawishi waumini wao wafuate maelekezo yao hususani masuala ya katiba inayopendekezwa au uchaguzi mkuu ujao, matamshi kama hayo yanakiuka sheria za usajili wa taasisi hizo”.

Amefafanua kuwa viongozi wa taasisi za dini wana haki ya kushiriki katika masuala ya kisiasa kama watu binafsi ila ni kinyume cha sheria kutumia uongozi wao kushawishi waumini wao watekeleze matakwa yao ya kisiasa.

“Aidha, waumini wa dini mbalimbali wana haki ya kuamini mafundisho ya dini zao lakini wanapaswa kutekeleza masuala yao ya kisiasa na kijamii kwa utashi wao wenyewe bila ya kushawishiwa na mtu yeyote, kama sheria za nchi zinavyotaka,” anasema.

Chikawe ametaja mfano mwingine akisema ni pale kiongozi au viongozi wa dini wanapochangisha fedha na kuandamana au kukutana na wanasiasa kwa kile kinachoelezewa kuwa ni kuwashawishi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.

Pamoja na kutowataja viongozi husika, bila shaka Chikawe aliwalenga baadhi ya wachungaji na masheikh kutoka mikoa mbalimbali ambao hivi karibuni walikusanyika kwa Lowassa na kumchangia fedha wakimwomba agombe urais.

“Serikali inapenda kuwataka wananchi mmojammoja au vikundi, zikiwemo taasisi za dini kuepuka kushiriki katika vitendo ambavyo vinaashiria kuvuruga amani na utulivu nchini. Serikali itachukua hatua za kisheria kudhibiti hali hiyo,” amesema Chikawe.

Ameongeza kuwa kuanzia wiki ijayo 20 Aprili mwaka huu, wizara yake itaanza kuvifuta vyama vyote vilivyosajiliwa chini ya sheria ya vyama, sura 337, ambavyo havifuati matakwa ya kisheria ya kuwasilisha taarifa zao za mwaka za ukaguzi wa hesabu na kulipa ada za kisheria.

error: Content is protected !!