July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yawaweka wananchi mguu sawa sensa ya 2022

Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imewaomba wananchi waachane na mila potofu wasikwamishe zoezi la sensa ya watu na makazi, litakaoiwezesha Serikali kuweka mipango bora ya kuwaletea maendeleo. Anaripoti Glory Massamu, TUDARCo … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Jumanne, tarehe 14 Septemba 2021, katika uzinduzi wa mkakati wa uelimishaji na uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi ya 2022, uliofanywa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, jijini Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango, amewasihi Watanzania wawe tayari kushiriki zoezi hilo litakapowadia, ili kuiwezesha Serikali kupanga maendeleo ya nchi.

“Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere, alitufundisha kwamba ili tuendelee moja ya vitu tunavyohitaji ni watu, zoezi hili la sensa linawezesha Taifa kujua idadi ya watu na nguvu kazi ya Taifa, jambo la msingi sana ili tuweze kupanga maendeleo ya nchi yetu,” amesema Dk. Mpango na kuongeza:

“ Pia wataalamu wa mipango wanasema ukishindwa kupanga umepanga kushindwa, kwa misemo hiyo miwili napenda kuwasihi Watanzania wenzangu wakati utakapofika kuhesabiwa, kila mmoja ajitokeze kuhesabiwa.”

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amewaomba wananchi wasiweke mbele imani potofu zitakakwamisha zoezi hilo.

“Hata sasa ulipokuja ugonjwa wa korona, UVIKO-19 ilipokuja chanjo wapo waliendelea kuwa baridi na wengine kupinga licha ya kutojua jambo hili linaweza kumfikia lini na mwisho wake litafikia wapi. Huku pia wakiwa hawana lililo na uhakika, hata upande wa sensa yamekuwa yakileta fikra potofu,” amesema Dk. Mwigulu.

Waziri huyo wa fedha amesema, Serikali imeamua kuandaa mkakati wa kuelimisha wananchi dhidi ya zoezi hilo, ili kuepusha dhana potofu kuhusu zoezi la kuhesabu watu.

“Zipo jamii, zilificha walemavu na kukataa watoto kuhesabiwa, tukaona kabla zoezi kuanza tupate kipindi cha kutosha kuelimisha na kutumia makundi yao, kama wafugaji waongee kifugaji, wakulima na vijana waongee kwa lugha yao ili sensa ifanikiwe,” amesema Dk. Mwigulu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili Zanzibar, Sera na Uratibu Zanzibar, Dk. Khalid Salim, amewoamba wananchi waiunge mkono Serikali katika zoezi hilo, kwa kuwa inatumia gharama kubwa.

“Kwa kawaida zoezi hili hutumia gharama kubwa ya rasilimali fedha na watu lakini Serikali imeridhia kufanyika zoezi hili, mkakati wa uelimishaji sensa ni moja wapo ya hatua ya maandalizi ya sensa itakayowezesha kuwa shirikishi kwa wadau wote,” amesema Dk. Salim.

error: Content is protected !!