November 30, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yawatangazia vita wanaotorosha madini

Spread the love

SERIKALI imewatangazia vita watu wanaotorosha madini ya Tanzanite pamoja na wanaokwenda kinyume na matakwa ya sheria. Anaripoti Regina Kelvin … (endelea).

Akizungumza jana tarehe 01 Agosti, 2018 wakati alipofanya ziara ya kutembelea migodi ya madini ya Tanzanite na ukuta wa Mirerani mkoani Manyara, Waziri wa Madini, Angellah Kairuki aliwaonya wezi wa madini hayo kwamba kiama chao kinakuja.

Waziri Kairuki amesema serikali itaendelea kusimamia ulinzi na kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo.

“Utoroshaji madini hausaidii, fedha ni za haraka lakini zinawaadhibu watanzania walio wengi kwa kuwa, fedha hizo hizo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo. Hivyo, kila mtanzania awe mlizi wa mwenzake,” amesema Kairuki.

Kwa upande wake,  Kamishna wa Madini, Mhandisi David Mlabwa, amesema  ni lazima Sheria, Kanuni na taratibu zizingatiwe wakati wa utekelezaji shughuli za uchimbaji madini kwa kuwa serikali inatambua mchango wa kila aina ya madini yanayopatikana nchini.

Naye, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Tumaini Magesa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kiteto amesema kuwa, shughuli za uchimbaji katika eneo la Mirerani zinaendelea na hivyo serikali itaendelea kuboresha ulinzi na kuhakikisha kwamba unaimalika.

error: Content is protected !!