Friday , 29 March 2024
Home Habari Mchanganyiko Serikali yatoa viwanda 10 viendelezwe, yawapa siku 21
Habari Mchanganyiko

Serikali yatoa viwanda 10 viendelezwe, yawapa siku 21

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imekabidhi kwa taasisi nne viwanda 10 ambavyo wawekezaji wake walishindwa kuviendeleza kulingana na mikataba ya mauzo hivyo malengo ya serikali ya kubinafsisha viwanda hivyo kutotimia. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea). 

Taasisi zilizokabidhiwa viwanda hivyo ni Mamlaka ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA), Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB).

Agosti 2021 Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, wakati huo alitangaza na kutoa maelekezo kuhusiana na viwanda 20 vilivyorejeshwa serikalini na kusema viwanda 10 vihamishiwe katika Taasisi za umma na 10 vitafutiwe wawekezaji wengine kwa njia ya zabuni.

Akikabidhi viwanda hivyo leo Ijumaa tarehe 27 Mei 2022 jijini Dar es Salaam, Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto amewapa wakuu wa taasisi hizo wiki tatu (sawa na siku 21) kuhakikisha wanawasilisha mpango kazi ambao utafuatiliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

“Ingawa leo nawakabidhi viwanda hivyo, mnatakiwa kuwasilisha mipango mikakati yenu ya kuendeleza viwanda hivi ifikapo 20 Juni 2022,” amesema Benedicto.

Amesema mipango hiyo ya uwekezaji watakayowasilisha ndiyo itatumika na Ofisi ya Msajili wa Hazina kufanya zoezi la ufuatiliaji na tathmini juu ya utekelezaji wake.

Msajili wa Hazina, Mgonya Benedicto

Viwanda 10 ambavyo vimeelekezwa kuhamishiwa katika taasisi hizo ni TPL Shinyanga Meat Plant ambacho ni cha nyama, Mafuta Ilulu (Lindi), kiwanda cha kubangua korosho cha Nachingwea Cashewnut (Lindi), Mkata Sawmill Limited na Sikh Sawmill Limited (Tanga), National Steel Corporation cha Dar es Salaam na  Mbeya Ceramic Ltd.

Vingine ni Mang’ula Mechanical & Machine Tools (Morogoro), Mwanza Tanneries (Mwanza) na TPL Mbeya.

“Kati ya viwanda hivyo, Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kitahamishiwa NDC, Kiwanda cha Mbeya Ceramic kinakwenda SIDO na Viwanda vinane vilivyobaki vinahamishiwa EPZA,” amesema Benedicto.

Amewataka viongozi wa taasisi hizo kuhakikisha wanatimiza malengo ya uwekezaji yakiwemo ya kuongeza uzalishaji, mapato kwa serikali, ajira, kuingiza teknolojia mpya katika sekta ya viwanda na uzalishaji na hatimaye kupunguza umasikini nchini.

Akifafanua zaidi amesema Kiwanda cha Mang’ula Mechanical & Machine Tools kinakabidhiwa NDC na  SIDO wamekabidhiwa Mbeya Ceramic huku viwanda saba vimekabidhiwa EPZA.

Viwanda vilivyokabidhiwa EPZA ni TPL Shinyanga Meat Plant, Mafuta Ilulu, Nachingwea Cashewnut, Mkata Sawmill Limited, Sikh Sawmill Limited, National Steel Corporation na TPL Mbeya.

Aidha, Benedicto amesema Kiwanda cha Mwanza Tanneries, Msajili atakabidhi viwanja vitatu (Na. 2,4, na 5) kati ya vitano  vilivyopo kwenye eneo hilo.

“Eneo lililobaki linasubiri maelekezo kutoka kwa mamlaka kabla ya kukabidhiwa rasmi kwa kuwa kulikuwa na maelekezo mengine ambayo yalitakiwa kukamilishwa kabla ya kufanya makabidhiano rasmi na EPZA” amesema.

Kuhusu Kiwanda cha TPL Mbeya ambacho kina eneo la Kiwanda (Plot Na. 760) na eneo la malishio ya wanyama (Nsalala Ground – Plot Na. 761), Msajili amesema atakabidhi eneo la Kiwanda tu huku akiendelea kusubiri maelekezo ya Serikali kuhusu Plot Na. 761.

Aidha, kwa upande wa Kiwanda cha National Steel Corporation, Ofisi ya Msajili wa Hazina imekabidhi eneo lililopo barabara ya Saza – Chang’ombe.

Msajili pia amesema kwa upande wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko anawakabidhi kinu cha kukoboa mpunga kilichopo Wilaya ya Kyela kwa ajili ya shughuli za ukoboaji.

Aidha walikabidhiwa ghala la mazao Wilaya ya Kiteto.

Awali, Mkurugenzi wa Ubinafsishaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mohamed Nyasama amesema taasisi hizo zimeaminiwa na Serikali, hivyo hazina budi kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza yale ambayo serikali inayatarajia katika kuimarisha uchumi wa nchi, lakini pia kusaidia ukuzaji wa ajira na kadhalika.

Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa taasisi zilizokabidhiwa viwanda hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa EPZA, Charles Itembe amemshukuru Msajili wa Hazina kwa kuwaamini na kuwapa jukumu la kufufua na kuendeleza viwanja ili viweze kuleta tija kwa taifa.

“Nchi inahitaji wawekezaji. Ndiyo maana hata Rais wa nchi anazunguka huku na huko kutafuta wawezekaji kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu kiuchumi. Tunajiona tuna deni kubwa serikalini lakini kwa tunaamini kwa juhudi za pamoja, tutahakikisha kazi hii inafanyika na kuweza kutimiza malengo ya serikali katika uwekezaji nchini,” amesema Itembe.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mazao Mchanganyiko, Dk Anselm Moshi, amesema wanashukuru kwa fursa na kwamba wanakwenda kutekeleza maagizo waliyopewa huku akiahidi nchi kuwa na hifadhi ya chakula cha kutosha.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari Mchanganyiko

Mtandao watetezi wa haki za mazingira Tanzania waundwa

Spread the loveMTANDAO wa watetezi wa haki za mazingira nchini Tanzania, umeundwa...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Kapinga kuongoza usambazaji wa mitungi ya gesi 10,000 ya Taifa Gas

Spread the loveNaibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga ameahidi kuongoza kwa ufanisi...

BiasharaHabari Mchanganyiko

Wafanyabiashara, wawekezaji China waridhia kuwekeza bil. 800 katika sekta 5 nchini

Spread the loveUJUMBE wa wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Jimbo la Changzhou...

Habari Mchanganyiko

Bil. 4.42 kumaliza uhaba maji kata 2 Musoma Vijijini

Spread the loveWANANCHI wa kata za Busambara na Kiriba, Jimbo la Musoma...

error: Content is protected !!