December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatoa tahadhari upungufu wa chakula, yatoa maagizo

Mahindi yaliyohifadhiwa kwenye viroba tayari kwa kwenda sokoni

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya upungufu wa mazao ya chakula unaosababishwa na ukame uliotokana na ukosefu wa mvua ya kutosha katika msimu wa 2021/2022. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Wito huo umetolewa leo Ijumaa, tarehe 11 Novemba 2022 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiahirisha shughuli za Bunge, jijini Dodoma.

Waziri Majaliwa amewataka wadau kuhifadhi chakula cha kutosha hadi pale mvua zitakapokuwa za kutosha.

“Kutokana na hali hiyo, ni vyema wadau wote kwenye masuala ya kilimo kuanza kuchukua tahadhari dhidi ya upungufu wa mazao ya chakula na kuhifadhi chakula cha kutosha mpaka hapo hali ya hewa itakapoanza kupata mvua ya kutosha,” amesema Waziri Majaliwa.

Kutokana na changamoto hiyo, Waziri Majaliwa ametoa maagizo manne kwa wadau wa sekta ya kilimo, ikiwemo kuendelea kutumia mbinu bora na himilivu kwa ajili ya kilimo endelevu kinachohimili ukame na chenye ufanisi, ikiwemo matumizi ya mbolea za mboji, samadi na kilimoo mtandazo kinachohifadhi maji kwenye udongo.

Pia, ameshauri wadau hao kupanda mbegu za mazao ya chakula yanayokomaa kwa muda mfupi na kutumia maji vizuri kwenye skimu za umwagiliaji.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Majaliwa amewaagiza maafisa ugani kushirikiana na vituo vya utafiti vilivyopo katika maeneo yao, kupata na kusambaza teknolojia za uzalishaji mazao.Pia, amewaagiza kutoa huduma za ugani kwa kuzingatia muongozo wa kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabia ya nchi wa 2017.

“Tuendelee kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu mkubwa, kuhifadhi chakula cha kutosha ngazi ya familia, kuepuka matumizi mabaya ya chakula au yasiyokuwa ya lazima kama vile utengenezaji pombe na matumizi mabaya ya chakula,” amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo, ilifanya tathimini ya kina ya hali ya upatikanaji chakula ngazi ya kaya katika maeneo yaliyobainika na upungufu wa uzalishaji chakula kwa msimu wa 2021/22.

Kufuatia tathimini hiyo, Waziri Majaliwa amesema Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), imetenga tani 4.5 milioni kwa ajili ya kupeleka katika maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa chakula, ambapo hadi kufikia Oktoba 2022, Halmashauri 20 zimepelekewa huduma hiyo.

Miongoni mwa halmashauri hizo ni, Liwale iliyopatiwa tani 200, Nachingwea (100), Bunda (400), Longido (1,872) na Handeni (100).

error: Content is protected !!