July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatoa maagizo kwa taasisi za dini, NGO’s

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeziagiza Taasisi za Dini na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), kufuata taratibu za kupata misamaha ya kodi, katika misaada inayopata kutoka kwa wafadhili wa nje ya nchi, kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi, tarehe 17 Juni 2021 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akimjibu Mbunge wa Kilolo (CCM), Justine Nyamoga, aliyehoji mkakati wa Serikali katika kukabiliana na vitendo vya urasimu, wakati wa taasisi hizo zinaposhughulikia misamaha ya kodi.

Akijibu ombi hilo, Waziri Majaliwa amezitaka taasisi hizo kufanya mapema taratibu za kuomba misamaha ya kodi, kabla ya mizigo yao kuingia nchini, ili kukwepa vitendo vya urasimu.

“Nitoe wito kwa taasisi ambazo zinapata msamaha, kwanza kueleza kikamilifu wanataka kuleta nini ambacho kinatakiwa kipate msamaha. Lakini bidhaa hiyo inayoletwa kwa msamaha lazima ikidhi matakwa ya Serikali, kwamba lazima kiende kikatoe huduma inayokusudiwa,” amesema Waziri Majaliwa.

Mbunge wa Kilolo (CCM), Justine Nyamoga

Waziri Majaliwa ameongeza “ kwa hiyo ili kuondoa urasimu, ni lazima taratibu zifuatwe mapema ili mzigo unapofika kwenye vituo, utoke mara moja.”

Aidha, Waziri Majaliwa amesema changamoto ya misaada ya wafadhili, kukwama kutolewa bandarini , mipakani au katika viwanja vya ndege, inapoingia nchini, inachangiwa na taasisi husika kutofuata taratibu za kupata misamaha ya kodi.

“Taratibu zimeandaliwa vizuri, suala la urasimu ambalo mbunge amelieleza inatokana pia na wale wenye bdihaa au mali inayoingizwa nchini. Kwa kutofuata utaratibu au kuratibu jambo zima bila kufuata utaratibu wake. Hilo linaweza sababisha uratibu wa muda mrefu,” amesema Waziri Majaliwa.

Pia, Waziri Majaliwa amesema taasisi hizo zimekuwa zikiingiza bidhaa tofauti na zile ilizoorodhesha kwenye maombi yao ya msamaha wa kodi.

“Lakini pia bidhaa hizi zinaposafirishwa nje ya nchi kuingia ndani, hao wenye bidhaa iwe taasisi ya kidini au yoyote inayopata msahama, lazima iwe imeandaa utaratibu wa kupeleka maombi. Pia kupeleka idadi ya orodha ya mali zinazoingia,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza:

“Uzoefu tulioupata serikalini ni watu wanaomba msamaha, lakini wanachokileta nchini sio kile alichokiombea msamaha. Kwa hiyo kunakuwa na hatua ndefu wengine wanasema urasimu serikalini, lakini hapana.”

Awali, Nyamoga alisema taasisi nyingi za dini zimekuwa zikikumbwa na changamoto hiyo, iliyosababisha waingie hasara ya kulipa gharama za kuihifadhi mizigo bandarini, kutokana na kuchelewa kutoka.

“Taasisi za dini zimekuwa zikikumbwa na adha kubwa ya vikwazo vingi na urasimu wakati wa kushughulikia misamaha ya kodi, wanapopata vifaa au misaada mbalimbali kutoka nje ya nchi,” amesema Nyamoga na kuongeza”

“Na kusababisha wakati mwingine vifaa hivyo kukaa muda mrefu bandarini na kuingia tatizo tena la stogare charges (gharama za kuhifadhi)na mwisho wake wanashindwa kuvitoa.”

error: Content is protected !!