July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatenga Sh. 1 trilion kusambaza maji

Spread the love

SERIKALI imesema imetenga kiasi cha sh 1 trilioni, kwa ajili ya kukarabati miradi ya maji katika miji 17 nchini ukiwemo mji wa Njombe na Makambako. Anaandika Dany Tibason, Dodoma … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni, na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge, alipojibu swali la nyongeza la mbunge wa Viti Maalum, Neema Mgaya (CCM) aliyetaka kujua ni lini serikali itatatua kero ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwame miji ya Njombe na Makambako.

Awali katika swali la msingi la mbunge huyo alitaka kujua serikali imejipangaje katika kutatua kero ya maji katika mji wa Makambako.

“Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika mji wa Makambako, Je serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo,” amehoji mbunge huyo.

Akijibu swali la nyongeza Mhandisi Lwenge amesema ni kweli kuna matatizo makubwa ya kero ya maji katika sehemu mbalimbali nchini.

Hata hivyo amesema kutokana na serikali kutambua kuwepo kwa kero hiyo serikali imetenga kiasi cha sh. 1 trilioni kwa ajili ya kukarabati miradi ya maji 17 nchini ukiwemo mji wa Njombe na Makambako.

Akijibu swali la msingi, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwere, amesema ujenzi wa mradi wa maji Makambako utatekelezwa katika awamu ya pili ya programu ya maendeleo ya sekta ya maji (WSDP11)katika mwaka wa fedha 2016/17.

Amesema kwa sasa serikali imekamilisha taratibu za kupata mkopo wa gharama nafuu kutoka serikali ya India kwa ajili ya utekelezaji miradi mingine ya maji.

Amesema katika mwaka wa fedha 2015/16 serikali ilitenga Sh. 1 bilioni ili kuboresha hali ya huduma ya maji katika mji wa Makambako.

error: Content is protected !!