SERIKALI imetenga Sh. 8 bilioni kwa ajili ya kuanzisha dirisha maalumu (Special Fund) litakalokuwa linasaidia watoto wanaotoka katika familia masikini. Anaripoti Erasto Masalu, Dar es Salaam … (endelea).
Akisoma Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2022/2023, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema dirisha hilo litaanzishwa chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia masikini.
Dk. Mwigulu amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kuanzisha dirisha hilo kupitia Tasaf baada ya kuguswa na watoto wanaokatisha masomo kwasababu mbalimbali ikiwemo kushindwa kupata mahitaji muhimu.
Waziri huyo alisema pamoja na serikali kuendelea kugharamia programu ya elimu msingi bila ada lakini wanafunzi wanakatisha masomo yao kutokana na umasikini wa kipato kwenye familia zao, mimba za utotoni, mwamko duni wa elimu kwa baadhi ya jamii na utoro na wale wasioendelea kwa mujibu wa sheria (Ufaulu).
“Ili kukabiliana na utoro (drop out) wa wanafunzi wanaotoka familia masikini, bado tuna watoto wanaoshindwa kumudu mahitaji ya lazima licha ya kuwepo kwa programu ya elimu bila malipo na hivyo wanasaidiwa na wabunge, madiwani na wengine kuchangiwa na wasamaria wema,” amesema Waziri Nchemba.
Waziri Nchemba amesema dirisha hilo litakuwa chini ya Tasaf kutokana na wao kuwa na mfumo wa kanzi data (database) ya watoto masikini wanaopatikana katika shughuli zao za kila siku.
Pia Waziri Nchemba amesema mbali na kanzidata ya TASAF watashirikiana na taarifa za wabunge na madiwani kutoka katika maeneo husika kupata watoto wanaotoka katika kaya masikini.
Leave a comment