April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatenga Bil 114.5 kumaliza changamoto ya maji Dar, Pwani

Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Maji na Umwagiliaji

Spread the love

SERIKALI imepanga kutumia kiasi cha Sh. 114.5 Bilioni katika kutekeleza miradi sita ya maji kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mikataba ya miradi hiyo leo tarehe 2 Julai 2019, Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Maji na Umwagiliaji amesema, miradi hiyo imelenga kuondoa changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama katika mikoa husika.

Prof. Mbarawa amesema, miradi mitano kati ya sita inatekelezwa kwa kutumia fedha za ndani, na mmoja unatekelezwa kwa mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia (W.B).

Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na usambazaji maji utakaoanzia maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam hadi Bagamoyo, mradi wa kusafirisha maji kutoka Jeti hadi Buza, usimamizi katika visima vya Kimbiji na Mpera, kusafirisha maji kutoka Mlandizi hadi Chalinze na Usambazaji maji kutoka Kisarawe hadi Pugu, na mradi wa maji katika mji wa Mkuranga.

Aidha, Prof. Mbarawa amezitaka mamlaka za maji nchini ziongeze juhudi katika ukusanyaji mapato ili ziweze kutekeleza miradi ya maji kwa kutumia fedha za ndani.

Suleiman Jaffo, Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) kazi nzuri inayofanya katika utekelezaji wa miradi ya maji, ambapo katika miradi sita ambayo mikataba yake imesainiwa leo, imechangia kiasi cha Sh. 40 Bilioni.

 “Dawasa inaongoza katika taasisi zote, leo hii tunasaini mikataba ya 114.5 Bilioni za mradi huo, kati ya hizo bil.40 ni mapato ya ndani ya Dawasa. Hayo mapato ya Dawasa ni sawasawa na bajeti ya wizara nyingine tunazo ziongoza,” amesema Jaffo.

Jumaa Aweso, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji ameitaka DAWASA kuhakikisha mita zake za mpya ambazo malipo yake yanafanyika kabla ya matumizi (Prepaid meters) zinawafikia wananchi ili kupunguza kero ya wananchi kulimbikiziwa bili za maji tofauti na matumizi yao halisi.

“Mimi nilipokuwa nimeteuliwa wizara ya maji nimefanya ziara Dar es Salaam wilaya zake zote, yote kuhakikisha tunasikiliza kero na namna gani tunazitatua, kero kubwa ni kuhusu suala la usomaji mita, kwamba zinakuja bili lakini zimekuwa na changamoto, “ amesema Aweso na kuongeza.

“Niwaombe sana Dawasa katika hili eneo la bili,  tumeona jitihada kubwa mnazofanya ya uanzishaji wa ‘Prepaid Meter’, zisambazeni kwa wananchi wote.”

error: Content is protected !!