July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatangaza kiama rushwa ukusanyaji kodi, maduhuli

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeonya kuwa itawafukuza kazi watumishi wa umma watakaobanika kufanya vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa fedha, hasa wakusanya mapato na maduhuli. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Onyo hilo limetolewa leo Jumanne, tarehe 14 Juni 2022 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/23, bungeni jijini Dodoma.

“Tunao uwezo wa kupangua safu nzima ya utumishi wa umma na tukapanga safu mpya ya vijana walioko mtaani, kwenye masuala ya uadilifu na uaminifu tusibabaishane. Tutawakamata tutawashtaki na kuwafunga. Lazima tukomeshe vitendo vya rushwa kwenye mapato na matumizi na jambo hili tutalifuatilia,” amesema Dk. Mwigulu.

Waziri huyo wa fedha, amesema baadhi ya watumishi wanaohusika na masuala ya uksuanyaji kodi na maduhuli ya Serikali, wamekuwa wakitumia zoezi la ukadiriaji kodi kwa wafanyabiashara, kuchukua rushwa kitendo kinachoikosesha Serikali mapato.

“Kuna vitendo vya rushwa kweye ukusanyaji mapato hasa kwenye kodi kubwa ya mapato ya mamlaka za Serikali za Mitaa na arhdi kuna mapato ya Serikali bado yanaingia kwenye mifuko ya watu binafsi. Hii inafanyika hasa panapotokea ukadiriaji wa viwnago vya juu ili kuruhusu majadiliano ya kwenda kwenye kodi stahiki yanayotakiwa kupunguzwa,” amesema Dk. Mwigulu.

Dk. Mwigulu amesema “Kiasi kinachopunguzwa chini ya kile anachostahili ndicho kinachopunguzwa na kuingia kwenye mifuko binafsi. Serikali imeshapokea taarifa kadhaa za matukio ya aina hii na inaendelea kufuatilia kwa makini jambo hili.”

Dk. Mwigulu, amewataka wananchi na wafanyabaishara kuwaripoti katika mamlaka husika, watumishi hao wanaowatishia kuwabambikia kodi ili wawape rushwa, akisema watashughulikiwa.

error: Content is protected !!