September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yatakiwa kuacha tafiti tegemezi

Spread the love

SERIKALI imetakiwa kuachana na mfumo tegemezi katika tafiti za kisayansi ili iweze kuwa na nguvu ya kupendekeza vipaumbele vyake vitakavyosaidia jamii kutokana na tafiti hizo, anaandika Regina Mkonde.

Hayo yamesemwa leo na Khadija Yahya-Malima, Mtafiti Mkuu Kitengo cha Afya katika Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) jijini Dar es Salaam.  

“ Serikali inatakiwa kufadhili tafiti kwa kushirikiana na wadau ili kuwezesha wanasayansi kufanya utafiti zitakazowasaidia kujua magonjwa kabla ya kujitokeza kwa jamii na au kufanya tafiti zitakazosaidia kuonesha watu mwenye viashiria vya magonjwa kwa lengo la kuwapatia kinga,” amesema.

Amesema, serikali ikijiondoa katika mfumo tegemezi kwenye tafiti za kisayansi na kujikita kwenye mfumo wa kujitegemea, itasaidia kuondokana na tafiti zenye mashinikizo ya kujibu tafiti za nchi nyingine pasipo tafiti hizo kutoa msaada kwa wananchi.

“Tunataka tafiti za afya zitakazosaidia jamii  kwa kutoa majibu ambayo yatasaidia jamii kuelewa ama kujua viashiria vinavyosababisha ugonjwa,” amesema Malima.

Aidha, amesema serikali itakapochangia kwenye tafiti kwa kushirikiana na wahisani itakuwa na uwezo wa kupendekeza vipaumbele vyake ili vifanyiwe utafiti.

“Serikali ikichangia fedha kwenye tafiti kwa kushirikiana na wahisani, itakuwa na mamlaka ya kutanguliza vipaumbele vyake ili vifanyiwe kazi katika tafiti husika,” amesema.

Mwelecela Malecela, Mkurugenzi na Mtafiti Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) amesema uhaba wa fedha ndiyo umekuwa chanzo cha kutokamilika tafiti nchini.

“Pesa ndiyo tatizo hususan katika tafiti za uvumbuzi kwa sababu zinachukua muda mrefu na kwamba wakati mwingine pesa hutumika nyingi pasipo tafiti hizo kuleta mafanikio,” amesema.

Ephata Kaaya, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) amesema tafiti zilizofanywa awali baadhi yake zilikuwa na mafanikio yaliyoisaidia jamii.

“Toka nchi ishirikiane na wahisani katika kufanya tafiti, baadhi yake zilileta mafanikio mfano kwenye utafiti wa ugonjwa wa malaria serikali iliweza kugundua kipimo cha haraka cha kuupima ugonjwa huo,” amesema.

Licha ya mafanikio hayo, Prof. Kaaya amesema kuwa kuna baadhi ya tafiti za magonjwa zilikuwa na changamoto ikiwemo ya ugonjwa Ukimwi kwa sababu watafiti walishindwa kugundua chanjo ya ugonjwa huo na kwamba kilichogunduliwa ni dawa za kupunguza makali.

 

error: Content is protected !!