
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako
SERIKALI ya Tanzania, imesema haitarudisha kikokotoo cha zamani cha mafao ya wastaafu cha asilimia 50, kwa kuwa hakileti usawa katika ugawaji wa fedha wanazopata wahusika, pamoja na kuathiri uhimilivu na ukwasi wa mifuko ya hifadhi ya jamii. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Hayo yamebainishwa leo Ijumaa, tarehe 24 Juni 2022, bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, akimjibu Mbunge Viti Maalum, Ester Bulaya, aliyeiomba Serikali iachane na kikokotoo kipya cha asilimia 33, akidai kinawaminya watumishi.
Bulaya aliiomba Serikali irudishe kanuni iliyokuwa inatoa mafao ya watumishi kwa mkupuo wa asilimia 50.
Hata hivyo, Prof. Ndalichako amesema, kikokotoo cha zamani cha asilimia 50, kilikuwa kinawapunja watumishi waliokuwa wanapata mafao ya mkupuo ya asilimia 25.
“Naomba nieleze athari zilizokuwa zinajitokeza kutokana na kanuni za mafao ya mkupuo wa asilimia 50, Ttnatoa mfano halisi, mchangiaji ambaye amechangia mfuko kwa miezi 467 na michango yake kwa muda wote wa utumishi ni Sh. 36 milioni, kanuni ya zamani ilikuwa inampa mafao ya mkupuo ya Sh. 129 milioni, yaani yeye amechangia Sh. 36 milioni lakini anapata mafao ya mkupuo ya Sh. 129 milioni,” amesema Prof. Ndalichako.
Prof. Ndalichako amesema “wafanyakazi wengine ambao wamechangia michango yenye thamani ya Sh. 86 milioni, amefanya kazi miezi 350 kwa kutumia mkupuo wa asilimia 25, anapata mafao ya mkupuo ya Sh. 54 milioni. Huyu amechangia milioni 36 analipwa 129. Huyu milioni 86 analipwa milioni 54.”
Prof. Ndalichako amesema kikokotoo kipya cha asilimia 33, kitaleta usawa kwa mafao ya watumishi “wale waliokuwa wanalipwa kidogo watakwenda kupata Sh. 74 milioni kwa kutumia kanuni mpya.”
Akizungumzia sababu ya kikokoto cha zamani kuathiri uhimilivu wa mifuko ya hifadhi ya jamii, Prof. Ndalichako amesema kilikuwa kinatoa mwanya kwa wastaafu kupata fedha nyingi za mafao, kuliko kiasi wanachochangia.
Amesema, changamoto hiyo pia ilitajwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
“Utaona kwamba ile fomula ilikuwa inampa mkupuo wa asilimia 50, ilikuwa haina uhalisia. Unachangia milioni 36 unalipwa mkupuo wa milioni 129 na hii imesababisha mifuko hali yake ya uhimilivu na ukwasi imekuwa ikiendelea kupungua mwaka hadi mwaka,” amesema Prof. Ndalichako na kuongeza:
“Na hii inajidhihirisha hata kwenye ripoti ya CAG ya Machi 2022, CAG anatuambia kwamba gharama za mafao zinazidi mapato ya michango hivyo kuhatarisha uwezo wa mifuko kulipa mafao.”
Kwa nini wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki iliyovunjika miaka ya 1970 bado hawajalipwa mafao yao?
Fedha zililipwa na Benki ya Dunia chini ya Dr. Victor Ubreit. Kenya ikapewa madeni.
Hii ya 50% na 33% haionyeshi kiasi cha riba kilichokuuza mapato yake.
Aliyewekeza mapema na kwa muda mrefu pato lake lilikuwa zaidi ya aliyewekeza kwa muda mfupi….tusiwaonee watu kwa mapato yao.
Watumishi wa muda mrefu ndio wanaosaidia uchumi wa nchi Tajiri wanapoenda sekta binafsi.
Tuache kuwanyanyasa na kuwanyima fedha zao. Ni haki zao!