December 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yataja sababu za kugomea mkataba wa AU hizi hapa

Dk. Damas Ndumbalo

Spread the love

SERIKALI imeeleza sababu za kutoridhia na kutia saini mkataba wa Jumuiya ya Afrika (AU) kuhusu masuala ya utawala bora, demokrasia na uchaguzi, ikisema kuwa, baadhi ya ibara za mkataba huo zinakinzana na katiba na sheria za nchi. Anaripoti Regina Mkonde … (endelea).

Sababu hiyo imeelezwa na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Damas Ndumbaro leo bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalum, Neema Mgaya aliyehoji sababu za Tanzania kutoridhia na kusaini mkataba huo ulioazimiwa na wakuu wa nchi mwanachama wa AU mwaka 2007.

“Nchi 35 tu zimeridhia mkataba huo, 19 bado haijaridhia ikiwemo Tanzania, Tanzania haijatia saini haijaridhia mkataba huo, na sababu zinazofanya isitie au ichelewe kutia saini, ni kuwepo ibara zilizo kinyume na katiba na sheria zetu. Katika kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa nchi inaangalia vigezo mbalimbali ikiwemo ukinzani wa mikabata hiyo na katiba na sheria yetu ya ndani,” amesema Dk.Ndumbaro.

Aidha, Dk. Ndumbaro amesema Tanzania inafanya mchakato wa ndani ili kuangalia namna ya kurekebisha sheria za ndani au kwenda kuiomba AU irekebishe vipengele vya mkataba huo vinavyokinzana na katiba na sheria za nchi, ili visikinzane.

“Tunafanya mchakato wa ndani kuangalia jinsi gani ya kurekebisha sheria za ndani au kwenda kuomba AU warekebishe vipengele ili viende sawa na sheria zetu, kisha tutasaini mkataba huo,” amesema.

Hata hivyo, Dk. Ndumbaro amesema licha ya Tanzania kutotia saini mkataba huo, bado masuala ya uchaguzi, demokrasia na utawala bora yanaratibiwa vizuri kwa mujibu wa katiba na kwa kuzingatia kanuni mbalimbali na sheria za uchaguzi pamoja na sheria za utawala bora.

Dk. Ndumbaro amesemaTanzania itaendelea kuheshimu demokrasia lakini pia itaendesha uchaguzi kwa uhuru na haki.

error: Content is protected !!