August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yasulubiwa bungeni

Aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu

Spread the love

KILE kinachonekana kuwa ni uamuzi wa kukurupuka, ndicho kinachoitoa jasho Serikali ya Rais John Magufuli bungeni leo, anaandika Aisha Amran.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeanza kuishinikiza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuomba radhi Bunge na Watanzania kwa ujumla kutokana na kuminya uhuru wa habari kinyume cha Katiba ya Nchi.

Joseph Mbilinyi, Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema hayo leo wakati akiwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusu bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17.

Kauli hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Dk. Vicent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema kueleza kwamba, chama hicho pamoja na vyama vingine katika muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) akieleza “tutatoka na mkakati kabambe wa kushughulika suala hili.”

Nape Nnauye, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na Michezo Januari mwaka huu alisoma tamko la serikali bungeni la kuondoa matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya bunge kupitia Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1) kwa madai ni gharama kubwa za uendeshaji ambapo baadaye vyombo vyote vilipigwa marufuku kurusha matangazo hayo jambo ambalo limezua mkanganyiko mkubwa.

Akiwasilisha makadirio hayo Mbilinyi amesema, Serikali ya Awamu ya Tano tayari imeanza vibaya kwa kuikanyaga haki na uhuru wa habari zilizotajwa kwenye Katiba ya Nchi na kwamba, ni dalili za dhahiri za utawala usiozingatia misingi ya kidemokrasia na kuwa ni utawala wa ki-imla.

“Licha ya mpango wa maendeleo wa Taifa kuonesha kwamba serikali itawekeza katika demokrasia, ikimaanisha kuwekeza katika mchakato wa uchaguzi, kupanua uhuru wa kujieleza, uwazi na kupatikana kwa taarifa lakini imeweka kando mpango huo na kuanza kutekeleza mpango mwingine wa siri wa kukandamiza uhuru wa habari.

“Serikali kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, imefuta moja kwa moja usajili wa gazeti binafsi la MAWIO kwa kipindi cha chini ya miezi sita toka imeingia madarakani,” amesema na kuongeza;

“… kwa kipindi hicho hicho imefuta asasi za kiraia zaidi ya 100 na haijatoa sababu za msingi za kufanya hivyo.

“Kana kwamba haitoshi, Serikali imezuia TBC1 Televisheni ya Umma, inayoendeshwa na kodi ya wananchi kurusha matangazo ya moja kwa moja ya mijadala inayofanyika Bungeni kwa kisingizio kwamba gharama za kufanya hivyo ni kubwa ambapo linatumia zaidi ya shilingi 4 bilioni kwa mwaka.”

Mbilinyi amesema, Serikali ya CCM imeendelea kuitumia sheria ya makosa ya mtandao ambapo vijana kadhaa wamefunguliwa mashitaka mahakamani kutokana na kutumia uhuru wao wa kikatiba wa kujieleza kupitia mitandao ya kijamii.

Amesema kwa kuwa mikutano ya Bunge ni muhimu kwa ajili ya wananchi kujua na kufuatilia utendaji wa wawakilishi wao ndani ya chombo hiki cha uwakilishi, na kwa kuwa serikali ilisitisha kwa amri TBC kutoendelea kurusha matangazo hayo ni dhahiri serikali ina sababu za ziada kuliko sababu za gharama.

“Ni dhahiri kuwa serikali haipo tayari kuona wananchi wakipokea matangazo ya moja kwa moja ya Bunge na inaelekea kuna sababu ambayo Kambi Rasmi ya Upinzani na wananchi kwa ujumla hawaijui kuhusu suala hili,” amesema Mbilinyi.

Amesema Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapenda kuweka msimamo wake rasmi kuwa, serikali imevunja Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18.

“Jambo hili ni la kulaaniwa na watu wote wapenda demokrasia ndani na nje ya Bunge hili,”amesema Mbilinyi.

Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo waandishi wa habari wameendelea kuwekewa vikwazo vya kisheria na kisiasa na kushambuliwa kimwili na kutishiwa maisha jambo linaloathiri utendaji wao na hivyo kuminya uhuru wa habari.

error: Content is protected !!