May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yasitisha sherehe za Nanenane

Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Kilimo

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imetangaza kusitisha sherehe za Maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane), kwa mwaka 2021 na kuagiza fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hizo, zitumike kuimarisha shughuli za ugani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Tangazo hilo limetolewa leo Jumatano tarehe 10 Februari 2021 na Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, jijini Dodoma. Maadhimisho hayo hufanywa tarehe 8 Agosti kila mwaka.

“Shughuli zote za Nanenane mwaka huu tumezifuta, kwa hiyo fedha zote za umma bila kujali ni wizara gani, zisitumike kwenye shughuli za Nanenane,” ametangaza Prof. Mkenda.

Waziri huyo mewaagiza viongozi na watendaji wa taasisi walioanza kufanya maandalizi ya sherehe hizo, kuacha mara moja.

“Kwa hiyo, Nanenane mwaka huu tumefuta, nawataka viongozi wote wa serikali na watendaji wote ambao sasa hivi wameanza kutumia posho kwenda kwenye mikutano, waache hizo safari. Waelekeze nguvu zao kwenye shughuli za ugani.”

“Nawasiliana na wizara nyingine zote zinazoshiriki katika shughuli ya Nanenane mwaka huu, kwamba fedha zote ambazo zilitakiwa zitumike kwa ajili ya hizo, hela yote hiyo ipelekwe katika kuimarisha shughuli ya ugani,” amesema.

Prof. Mkenda amesema, serikali imechukua hatua hiyo ya kuelekeza fedha za Nanenane katika shughuli za ugani, baada ya kubaini shughuli hizo zinasuasua kutokana na ukosefu wa fedha.

“Sababu hakuna sababu ya kuweka afisa ugani kule wakati hatujatengeneza mazingira ya wao kuwasaida wananchi, wako wakulima wanakuambia mimi sijui napataje huduma ya ugani,” amesema Prof. Mkenda.

Amesema, kwa mwaka huu wizara yake kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya kilimo, watafanya tathimini ya kubaini namna ya kuendesha maonesho hayo katika miaka ijayo, ili kuhakikisha yanaleta tija kwa wakulima.

“Tutafanya tathmini vizuri namna ya kuendeleza shughuli za Nanenane, tunataka tuendeleze, haya maonesho ni mazuri sio mabaya, lakini tutaanzisha taskforce (kikosi kazi) kuhakikisha kwamba tuna maonesho yenye impact (faida),” amesema Prof. Mkenda.

Prof. Mkenda amesema, changamoto za shughuli za ugani nchini zilibainika katika kikao cha siku mbili kati ya Wizara ya Kilimo na maofisa ugani wa nchi nzima, kilichofanyika tarehe 29 Januari 2021.

“Hii ripoti ambayo nimepokea baada ya kikao chetu na maafisa ugani cha siku mbili nchi nzima, hayo ndio nilitaka nitangaze kwamba Nanenane mwaka huu hakuna na tutatumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kuendeleza zaidi ya shughuli za ugani,” amesema Prof. Mkenda, ambaye pia ni mbunge wa Rombo (CCM).

Amesema katika kikao hicho, changamoto za sekta ya ugani ziliorodheshwa kisha akakabidhiwa ripoti yake, ambayo amejipanga kuifanyia kazi.

“Tuna taarifa nzuri sana tumeipata baada ya mkutano wetu kuhusu shughuli ya ugani, changamoto gani tunahitaji tuzitatatue, najua hatutamaliza zote, lakini tunataka tuanze safari ya kutatua hizi changamoto,” amesema Prof. Mkenda.

Nje ya kufuta maonesho ya Nanenane ya 2021, Prof. Mkenda amesema, wizara yake itabadilisha matumizi ya fedha ambazo zilitengwa katika maeneo yasiyokuwa na umuhimu, kisha kupeleka kwenye maeneo yenye matokeo makubwa, ikiwemo ugani.

“Sehemu mojawapo kama nilivyosema, kujaribu kuhamisha fedha kwenye baadhi ya maeneo na kupeleka katika maeneo yenye impact (faida) kubwa,” ameahidi Prof. Mkenda.

error: Content is protected !!