SERIKALI ya Tanzania imerejesha mfumo wa zamani wa ununuzi wa mazao ya kimkakati, ili kuondoa changamoto za mfumo wa soko huria. Anaripoti Nasra Bakari, DMC … (endelea).
Taarifa hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe18 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma na Naibu waziri wa Kilimo, Hussen Bashe, akimjibu Innocent Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa mkoani Kagera, aliyehoji mkakati wa Serikali katika kutatua changamoto ya ucheleweshaji malipo kwa wakulima wa kahawa.
Akijibu swali hilo, Bashe amesema baada ya mabadiliko hayo, wakulima watauza mazao yao kupitia vyama vyao vya ushirika.
“Kutokana na changamoto za mfumo wa soko huria, Serikali ya Awamu ya Tano iliamua kurejesha ununuzi wa mazao matano ya kimkakati (Korosho, Tumbaku, Pamba, Kahawa na Chai), kupitia Vyama vya Ushirika ili kunufaisha wakulima, wanunuzi , wafanyabiashara na Serikali kwa ujumla,” amesema Bashe.

Kuhusu changamoto ya wakulima wa Kahawa mkoani Kagera kuchelewa kulipwa fedha zao, Bashe amevitaka Vya vya Ushirika (AMCOS), kutafuta masoko ya uhakika mapema ili kuondoa changamoto hiyo.
“Katika mfumo wa soko la kahawa Serikali hainunui kahawa bali imeweka mfumo wezeshi kwa wakulima kuuza mazao yao kupitia mfumo wezeshi wa wakulima kuuza mazao yao kupitia mfumo wa ushirika ambapo wanunuzi binafsi wameruhusiwa kununua kahawa kupitia AMCOS,” amesema Bashe na kuongeza:
“Mwongozo wa Bodi ya Kahawa unaelekeza kuwa wakulima walipwe ndani ya siku tatu pindi AMCOS inapofanya makubaliano na kampuni yenye leseni ya kununua kahawa.
Aidha, Vyama vya Ushirika vimeshauriwa Kutafuta masoko mapema ili kuwezesha kupata fedha kutoka taasisi za fedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) au wanunuzi wanaoingia nao mikataba ili kuwezesha kulipa wakulima pindi wanapoleta kahawa kwenye Vyama vyao vya msingi.”
Leave a comment