June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yapongezwa kufuta mfumo wa GPA

Spread the love

SHIRIKISHO la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi nchini (TANGOSCO) limeipongeza Serikali kwa  kuondoa mfumo wa GPA na kurejesha madaraja katika matokeo ya mitihani kwenye shule za sekondari, hasa kwa kidato cha pili na cha nne. Anaandika Regina Mkonde … (endelea).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mrinde Mzava, mwenyekiti wa TANGOSCO, amesema mfumo wa GPA umekuwa unakanganya wazazi na kuwafanya washindwe kujua ufaulu sahihi wa watoto wao.

Amesema mfumo huo umedumaza kiwango cha elimu na kushusha viwango vya wanafunzi kwa sababu wamekuwa wanasukumwa kupanda madarasa bila ya kuzingatia ufaulu wao.

“Waziri ameitendea haki jamii ya kitanzania kwa kuurudisha mfumo unaoeleweka na kukomaza viwango vya elimu nchini, hususani (katika) kipindi hiki ambacho nchi yetu imekuwa ya mwisho kwenye ukanda wa Afrika Mashariki katika kutoa wahitimu wenye wenye elimu bora. Pia wasomi wetu hawana viwango vizuri vya kupambana kwenye soko la ajira la nje ya nchi,” amesema na kuongeza:

“Wanafunzi wengi wa kidato cha pili wanaingia kidato cha tatu ingawa hawana ufaulu mzuri. Wanasukumwa ili mradi wawe wameingia kidato cha tatu. Hali hii ni sawa na kuhujumu jitihada za wazazi na walezi. Wazazi wanajitoa kusomesha watoto wao ili wapate elimu bora. Kitendo cha mwanafunzi kumaliza shule ilhali hana elimu yenye kiwango itakayomsaidia kushindana kwenye soko la ajira ni sawa na kumhujumu mzazi.”

Wadau wa elimu, hasa wamiliki wa shule na vyuo binafsi nchini, wamekuwa wanalalamikia mfumo wa GPA tangu ulipoanza kutumika katika miaka mwili ya mwisho ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete.

Wanadai kwamba matumizi ya mfumo wa GPA yamerudisha nyuma maendeleo ya wanafunzi kwa kuwadekeza na kupunguza juhudi za kujifunza, kwa sababu hata waliofeli hujumuishwa na waliofaulu.

Vile vile, wanasema mfumo wa GPA haukidhi viwango vya soko la ajira za nje ya nchi. Baadhi yao wamekuwa wanasema GPA ni sawa na kupanua magoli ili timu inayoshindwa kufunga magoli ipate ifunge kirahisi.

Mwanzoni mwa wiki hii, Profesa Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu na Ufundi Stadi, amefuta mfumo wa GPA na kutaka Baraza la Mitihani la Taifa lirejeshe mfumo wa zamani wa kutumia madaraja kutangaza matokeo ya mitihani.

Hata hivyo, wakati TANGOSCO inampongeza waziri, tayari matokeo ya kidato cha pili ya mwaka jana yalikuwa yameshatolewa kwa mfumo wa GPA.

Naye Fidelis Mwampoma, mwenyekiti wa wakuu wa shule zisizo za serikali, alisema wazazi wengi hupeleka watoto wao shule za binafsi kwa sababu wanaamini kuwa ndizo hutoa elimu bora, na kwamba serikali ya awamu ya nne ilipoanzisha mfumo wa GPA ililenga kukomoa shule za binafsi kwa kuwa zinafanya vizuri, ili zifanane na za serikali katika ubora wa elimu.

Alisema pia kwamba serikali inapobadilisha mifumo kila mara inachangia kudumaza elimu na kupoteza dira ya elimu nchini. Aliitaka iige mfumo wa elimu wa Kenya ambao umedumu kwa muda mrefu, jambo lililochangia nchi hiyo kuwa na viwango vizuri vya elimu ikilinganisha na viwango vya Tanzania.

“Kitendo cha Serikali kubadilisha mifumo kila mara kimechangia kushusha kiwango cha elimu, mfano mzuri ni Kenya. Imedumu kwenye mfumo wa elimu ulioachwa na mkoloni lakini hadi sasa ina viwango vizuri na wahitimu wake wanafanya vizuri kwenye soko la ajira,” alisema Mwampoma.

Mwampoma aliitaka serikali iboreshe mazingira ya elimu na waalimu kwani ili elimu bora ipatikane, ni lazima waalimu waandaliwe masilahi na mazingira mazuri ya kazi.

error: Content is protected !!