SERIKALI nchini Tanzania imepongeza uwekezaji uliofanywa na Mtandao wa Elimu ya Afya Kairuki (KHEN), kwenye sekta ya elimu ya afya kwani unachangia juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar….(endelea)
Pongezi hizo zilitolewa jana Alhamisi tarehe 9 Juni na Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, wakati wa kongamano la kisayansi lililofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert kairuki (HKMU), Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri amesema uwekezaji uliofanywa na Hayati Profesa Kairuki kwenye sekta ya afya ni mkubwa na wa kuigwa kwani umesaidia kupunguza msongamano kwenye hospitali za serikali.
Amesema Mtandao huo umekuwa na mchango mkubwa kwenye sekta ya afya kwa kuanzisha Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), ambacho kimekuwa kikitoa idadi kubwa ya wataalamu wa sekta ya afya.
“Sayansi ndiyo jicho la taifa lolote duniani hivyo mchango wenu kwenye kuzalisha watalamu wa afya ni mkubwa sana na serikali inathamini kazi kubwa mnayofanya serikali itaendelea kuwasaidia na kuwaunga mkono,” amesema Dk. Mollel.
Amesema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye sekta ya afya na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameshatoa Sh bilioni nne kwa Taasisi ya Utafiti wa Afya (NIMRI), ili waweze kutafuta chanjo za kukabiliana na magonjwa mbalimbali.
Amesema wanasayansi lazima wajipange kukabiliana na magonjwa yatokanayo na virusi kwani dalili zinaonyesha kwamba ndilo tishio kubwa duniani kwa siku zijazo.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Yohana Mashalla, amesema magonjwa ya kuambukiza yamekuwa changamoto kubwa sana kwa nchi zinazoendelea kulinganisha na zile zilizoendelea.
Amesema mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 umeonyesha ni kwa namna gani taifa linapaswa kuweka mifumo imara kujiandaa kukabiliana na majanga ya aina hiyo yatakapotokea siku za mbele.
“Iko haja ya kuimarisha mifumo yetu ya afya ili tuweze kujitayarisha kukabiliana na maradhi ya mlipuko kama COVID 19 na lazima tufahamu kuwa COVID siyo ya kwanza na wala siyo ya mwisho kuna milipuko itakuja tujiandae,” amesema
Leave a comment