August 12, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yapiga marufuku udalali wa ardhi

Spread the love

SERIKALI wilayani Kilosa imepiga marufuku tabia ya udalali wa ardhi na badala yake anayehitaji ardhi kufuata sheria na taratibu za umiliki wa ardhi lengo likiwa ni kuthibiti migogoro ya ardhi, anaandika Christina Raphael, Kilosa.

Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na John Henjewele Mkuu wa wilaya ya Kilosa wakati wa mkutano wake na wanakijiji wa kijiji cha Mabwerebwere, maofisa mawasiliano wa serikali, waandishi wa habari katika ziara ya kutokomeza mapigano kati ya wakulima na wafugaji wilayani Kilosa.

Henjewele alisema kuwa migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kiasi kikubwa inachangiwa na tabia ya udalali wa ardhi unaofanywa na wakulima au madalali ambao wamekuwa wakishikilia kiasi kikubwa cha ardhi ambacho hawakitumii na badala yake wamegeuza kuwa kufanyia biashara.

Amesema kuwa madalali hao wengi ni wazawa wa kijiji hicho na wamehodhi maeneo makubwa aambayo baadaye huyatumia kwa udalali kuwakodisha wafugaji ambao wakati huohuo ardhi hiyo wanakuwa wameshaitoa kwa wakulima na matokeo yake ni kuibuka kwa migogoro.

Amesema kuwa hatua za kuwawajibisha watu hao tayari zimekwishaanza na kwa kuanzia wanaanza na kijijicha Mabwerebwere kijiji ambacho ni kitovu cha migogoro baina ya wakulima na wafugaji .

Migogoro ya wakulima na wafugaji imedumu zaidi ya miaka 20 wilayani kilosa na mpaka sasa hakuna ufumbuzi wowote unaofanyika kukabiliana na mogogoro hiyo wilayani humo.

error: Content is protected !!