July 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaonya watu, NGO’s zinazochochea mgogoro Ngorongoro

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imetangaza kusudio la kuwachukulia hatua watu pamoja na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’s), yanayochochea mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Onyo hilo limetolewa leo Ijumaa, tarehe 10 Juni 2022, bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akitoa kauli ya Serikali kuhusu video ilizosambaa katika mitandao ya kijamii, ikionesha baadhi ya wakazi wa Loliondo wilayani Ngorongoro, wakitishia kurushiana mishale chanzo kikidaiwa kuwa ni mgogoro huo.

“Tunatambua ziko taasisi tumezisajili ambazo zinazojihusisha na uhifadhi lakini katika hili inaonekana mara nyingi kazi yao kupotosha na kuchonganisha kati ya raia wanaokaa katika eneo lile, ambao ni wafugaji na Serikali,” amesema Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema, Serikali iko macho dhidi ya watu wanaochochea mgogoro huo, ikiwemo kuwahasisha wananchi walioko katika eneo wanalopaswa kuondoka kwa hiari kugoma kutekeleza agizo hilo.“lakini nataka niwaambie, Serikali iko macho dhidi yao, hatutamuonea mtu yeyote yule.”

Akizungumzia video hiyo iliyosambaa hasa katika mtandao wa Twitter, Waziri Majaliwa, alisema ni mkakati unaofanywa na baadhi ya watu kuichafua taswira ya Tanzania.

“Video zilizorushwa ilikuwa mkakati wa kutengeneza kuleta taswira mbaya ndani ya nchi na nje ya nchi. Lakini kimsingi hakuna mapambano yoyote. Hakuna askari aliyekwenda huko kijijini kwenda kutishia kwa namna yoyote ile,” amesema Waziri Majaliwa.

Naye Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameshauri vyombo vya kisheria viwachukulie hatua watu pamoja na taasisi zinazochochea mgogoro huo.

“Kwa sababu upotoshaji umeanza muda kidogo, Serikali imekuwa ikifafanua na kwenda kwenye ziara ikitoa habari. Lakini jambo hili linaendelea sababu hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wanaofanya hasa walioko nchini sababu tunafahamu tuko kwenye vita ya kiuchumi na nchi nyingine,” amesema Spika Tulia na kuongeza:

“Kama kuna mtu anafanya upotoshaji kama aliyechukua video, tunaweza tukaanza na huyo halafu wengine wanafuata ikiwa ni pamoja na hizi taasisi ambazo zimesajiliwa nchini kwetu tukifikiri zina lengo jema na sisi. Kama zinafanya tofauti sheria zichukue mkondo wake.”

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutatua mgogoro huo ulioko kwenye Kata za Sale, Loliondo na Ngorongoro, Waziri MKuu Majaliwa amesema, wananchi wa vijiji 14 vya Loliondo, hawatahamishwa badala yake Serikali imeweka utaratibu mzuri wa wao kubaki hifadhini hapo bila kuathiri uwepo wake.

“Lile eneo (Loliondo) kama tutatumia mifugo ya Watanzania tu, linaweza kuratibiwa vizuri zaidi na litakuwa chanzo endelevu. Lakini tukiruhusu kuongeza idadi ya mifugo kutoka popote pale litapotea.”

Tunaamini wale wote wanaohamasisha vibaya wananchi wale wataacha mara moja kufanya hivyo ili kuwafanya wananchi waendele na shughuli zao bila kupoteza amani,” amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema, hadi sasa Serikali imejenga nyumba za makazi 103 ambazo ziko ndani ya eneo la hekari tatu kila moja wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga.

Amesema katika makazi hayo, kuna maeneo ya malisho ya mifugo, visima vya maji vitatu vinavyofanya kazi, kituo cha afya, shule ya msingi na sekondari, pamoja na miundombinu mingine muhimu.

Majaliwa amesema, hadi sasa kaya 293 zenye watu 1,497 zinazoishi katika Hifadhi ya Ngorongoro, zimekubali kuhama kwa hiari kwenye hifadhi hiyo ambapo mabasi ya kuwabeba, malori ya mizigo na mifugo kwa gharama za serikali yataandaliwa pamoja na kulipwa fidia.

Amesema Serikali itagharamia shughuli za kuwahamisha wananchi hao kutoka Ngorongoro hadi Handeni, mkoani Tanga.

“Mpaka jana jioni kaya 293 zenye watu 1,497 wamejiandikisha kwa hiari yao. Idadi hii ya watu tunapeleka Kijiji cha Msomera wilayani Handeni, Tanga.”

“Hatujaanza bado sababu Serikali ilijipanga kuandaa mazingira mazuri ya wao kusihi pamoja na ujenzi wa nyumba. Mpaka leo tumejenga nyumba 103 na zimekamilika kwa asilimia 100,” amesema Majaliwa.

error: Content is protected !!