August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Serikali yaonya vyama vya ushirika

Spread the love
WANAOANZISHA Vyama vya Ushirika kwa lengo la kupata fedha za misaada na kutelekeza vyama hivyo, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kulipa faini na kifungo cha miaka mitano jela, anaandika Regina Mkonde.
Hayo yamesemwa leo na Dk. Audax Rutabanzibwa, Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Kifungu cha sheria namba 123 ya mwaka 2013 kinasema kuwa kuanzisha chama cha ushirika kwa lengo la kupata fedha kisha kukitelekeza, ni kosa la jinai na kwamba faini yake ni milioni tano na kufungwa kifungo cha miaka 5,” amesema.
Amesema kuwa, sambamba na adhabu ya faini na kifungo, Rutabanzibwa amesema kuwa atakayebainika kufanya kosa hilo atafilisiwa mali zake zote.
Hatua hiyo inaenda sambamba na hatua ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika ya kukusudia kuvifuta katika daftari la vyama vya ushirika vyama ambavyo vimekiuka matakwa ya sheria ya vyama vya ushirika Na. 6 ya mwaka 2013.
Akizungumzia kuhusu kufutwa kwa vyama hivyo, Rutabanzibwa amesema vyama vinavyokusudiwa kufutwa ni 1,862 na kwamba vitafutwa baada ya siku tisini kuanzia tarehe 13 Mei, 2016.
“Kwa mujibu wa sheria, Mrajis wa vyama vya ushirika kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu Na. 11, 8 na 100 anatakiwa kuvifuta vyama ambavyo vimeshindwa kufanya kazi katika kutimiza masharti ya usajili wake,” amesema.
Amefafanua baadhi ya masharti hayo yaliyokiukwa ikiwa pamoja na  kutofanyika kwa mikutano,kutokufanyika kwa chaguzi za viongozi kwa mujibu wa sheria, idadi pungufu ya wananchama na kutofanyika kwa shughuli za kichama kwa zaidi ya miezi sita.
“Mtu yeyote au taasisi yenye pingamizi la msingi dhidi ya kufutwa kwa chama husika, anatakiwa awasilishe pingamizi hilo na sababu zake katika ofisi ya Mrajis kupitia Warajis wasaidizi wa mikoa husika ndani ya siku tisini,” amesema.
Amesema Tume ya Vyama vya Ushirika inadhamiria kuvifanya vyama vya ushirika kuwa sehemu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kwamba hapo awali vyama hivyo vilishindwa kuchangia pato la taifa kutokana na ubovu wa uongozi.
“Ukweli ni kwamba usimamizi mbovu, kutokuwepo kwa mpango biashara ni sehemu ya sababu iliyopelekea vyama hivyo kutoleta maendeleo kwa wanachama wake na kutoliingizia Taifa mapato ya kutosha,” amesma.
Jumla ya vyama vya ushirika vilivyopo nchini ni 8040, na kwamba kati ya hivyo vyama vya kilimo ni 2,918, akiba na kilimo 4098 huku vilivyobakiwa vikiwa vyama vya makundi tofauti tofauti.
error: Content is protected !!